1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama ajipatia ushindi mkubwa.

21 Mei 2010

Wabunge waliupitisha kwa kura 59 dhidi ya 39

https://p.dw.com/p/NTiM
Rais Barack Obama ajipatia ushindi baada ya kupitishwa kwa muswada wa marekebisho ya kiuchumi.Picha: AP

Wabunge waliupitisha muswada huo kama njia ya kuyadhibiti matumizi ya fedha ya ziada yanayolaumiwa kusababisha mzozo wa kiuchumi wa mwaka 2008.

Kiongozi wa Wademocrat wenye wingi katika baraza la Seneti, Harry Reid alisema kwa soko la hisa, hatua hiyo inamaanisha kwamba halitoweza tena kucheza kamari kwa kutumia fedha za umma.

Muswada huo ambao ulikuwa lengo kuu la kitaifa la rais Obama sasa lazima uainishwe na pendekezo la baraza la wawakilishi kabla ya hatua ya mwisho ya kutiwa saini na rais ili uwe sheria.

Mwenyekiti wa kamati ya huduma za fedha ya baraza la wawakilishi kutoka chama cha Democrats, Barney Frank alisema katika mahojiano na shirika la utangazaji la CNBC kwamba alitabiri mambo yangekuwa shwari na ana uhakika kwamba rais atakuwa ametia saini muswada huo kabla ya tarehe 4 Julai.

Hatua hiyo inaazimia kudhibiti mikakati hatari ya mashirika makubwa inayolaumiwa kusababisha mzozo wa kiuchumi wa mwaka wa 2008, kusitisha mfumo wa kulipa madeni kwa kutumia fedha za watozwa kodi na hatimaye kuunda wakala utakaowalinda wamarekani dhidi matumizi mabaya ya fedha.

Wall Street / Börse / Dow Jones
Muswada huo unanuia kudhibiti taasisi za fedha.Picha: AP

Jarida la Wall Street limeripoti kwamba hatua hiyo itapunguza faida za taasisi za fedha kwa takriban asilimia 20.

Muswada huo unajumuisha pia hatua kadhaa zinazolenga kuongeza uwazi zaidi katika benki ya akiba ya Marekani na uwajibikaji katika benki kuu,pamoja na kuzuwia mipango ya utoaji misaada ya shirika la fedha la kimataifa kama ule wa kuokoa Ugiriki ambapo hakuna hakikisho kama fedha zilizopewa zitalipwa.

Muda mfupi kabla ya kura kupigwa, Rais Obama alitoa hutuba ya mwisho kwa wajumbe akiwataka kuungana na kuwashinda wakosoaji wanaosema kwamba muswada huo utaliathiri soko. Alisema kwa sababu ya marekebisho ya kiuchumi, Wamarekani hawatawahi kuulizwa kulipa gharama yatakayotokana na makosa katika soko la hisa na kwamba fedha za walipa kodi hazitatumiwa kukwamua uchumi. Aliongeza kusema kwamba ikiwa taasisi kubwa ya kiuchumi itashindwa kuwajibika, watakuwa na njia ya kukabiliana nayo bila ya kutishia uchumi kwa jumla.

Waziri wa fedha wa Marekani, Tim Geithner alisema kwamba anatarajia kushirikiana na wabunge ili kufanya marekebisho mahasusi yatakayoiweka imara mfumo wa fedha wa Marekani na pia kuweka mazingira mazuri ya ushindani katika uchumi duniani.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed