1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Haki sawaUganda

Benki ya Dunia yakemea sheria ya Uganda dhidi ya mashoga

9 Agosti 2023

Benki ya Dunia imesema itasitisha utoaji wa mikopo mipya kwa serikali ya Uganda baada ya kuafiki kuwa sheria ya nchi hiyo dhidi ya jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja inakinzana na maadili ya Benki hiyo.

https://p.dw.com/p/4Uw1G
Uganda l LGBTQ
Picha: uncredited/AP/picture-alliance

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, Benki hiyo imesema hakuna ufadhili mpya wa umma utakaotolewa kwa Uganda hadi hatua za ziada na za ufanisi zitakapochukuliwa, na kuongeza kuwa hatua hizo sasa zinajadiliwa na mamlaka za Kampala.

Ujumbe wa Benki ya Dunia ulisafiri hadi Uganda mara baada ya kuanzishwa kwa  sheria hiyo dhidi ya mashoga  na ambayo imekuwa ikikosolewa na mataifa kadhaa pamoja na Umoja wa Mataifa. Wajumbe hao waliamua kwamba kulihitajika hatua za ziada kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia kanuni za kijamii na kimazingira za taasisi hiyo.

Indien | Ajay Banga
Rais mpya wa Benki ya Dunia Ajay Banga, aliyechukua wadhifa huo Juni,2023.Picha: Punit Paranjpe/AFP/Getty Images

Rais mpya wa Benki ya Dunia Ajay Banga, aliyechukua wadhifa huo mwezi Juni na ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kutoa msimamo wake juu ya sheria hiyo, amesema sheria ya kupinga ushoga ya Uganda kimsingi inakinzana na maadili ya Benki ya Dunia, na kuongeza kuwa anaamini kwamba maono ya kutokomeza umaskini Ulimwenguni yanaweza kufanikiwa ikiwa tu yatawajumuisha watu wote bila kujali rangi yao au jinsia.

Soma pia: UN: Uganda lazima ifute sheria yake mpya ya kupinga ushoga

Museveni aitetea sheria ya kupinga ushoga

Banga amesema bado wana nia ya kuendelea kuwasaidia Waganda wote kuepuka umaskini, kupata huduma muhimu, na kuboresha maisha yao lakini bila kumtenga yeyote. Mnamo Juni 15 mwaka 2023, jumla ya vikundi 170 vya kiraia vilimtaka Banga kuchukua "hatua mahususi, madhubuti na kwa wakati" ili kujibu sheria ya Uganda dhidi ya jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ) ikiwa ni pamoja na kusitisha mikopo ya baadaye kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

 Hadi mwishoni mwa mwaka 2022, Benki ya Dunia ilitoa kitita cha dola bilioni 5.4 kufadhili miradi ya maendeleo nchini Uganda ikiwa ni pamoja na miradi mingi ya afya na elimu ambayo inaweza kuathiriwa na hatua hii mpya.

Baadhi ya misaada ya maendeleo kuendelea kutolewa

Uganda führt drakonisches Anti-Schwulengesetz ein
Bunge la Uganda likijadili muswada wa sheria dhidi ya mashoga (LGBTQ): 21.03.2023Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hata hivyo chanzo cha Benki ya Dunia kimebaini kuwa Mfuko wa Ufadhili wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa kwa Uganda utaendelea kutoa fedha kwa nchi hiyo bila kujali hatua ya kusitisha mikopo mipya.

soma pia: Museveni akaidi miito ya kumtaka afute sheria dhidi ya ushoga

Benki hiyo imeendelea kuwa miradi ya sekta binafsi inayoungwa mkono na Shirika la Kimataifa la Fedha na Wakala wa Dhamana ya Uwekezaji wa Kimataifa (MIGA) itaendelea lakini kwa kuchujwa, na kuongeza kuwa miradi hiyo pia itazingatia hatua za kuhakikisha ujumuishwaji na kutomtenga yeyote na kwamba itaimarisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa ufuatiliaji na malalamiko ya watu wa Uganda.

Sheria mpya ya Uganda inatoa hadi hukumu ya kifo kwa kile kinachotajwa kuwa "ushoga uliokithiri" kosa linalojumuisha kusambaza Virusi Vya Ukimwi kupitia ngono ya mashoga.

(RTRE,APE)