1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Berlin kusaka mwarobaini utekelezaji ukomo wa deni

24 Novemba 2023

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner amesema serikali mjini Berlin inatafuta njia za kusimamisha kwa mwaka wa nne mfululizo utekelezaji wa ibara ya katiba inayoweka ukomo wa deni la taifa.

https://p.dw.com/p/4ZOUx
Taarifa ya waziri wa fedha Christian Lindner
Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian LindnerPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Dhamira hiyo imetangazwa baada ya mahakama ya shirikisho kuizuia serikali kuchukua mkopo mkubwa wa kufadhili miradi ya kimkakati, uamuzi uliozusha mparaganyiko kwenye mipango ya bajeti ya mwaka ujao. 

Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner ameandika katika mtandao wake wa kijamii kuwa, serikali ya shirikisho itawasilisha bajeti ya ziada ili kulinda kikatiba matumizi ya fedha ya mwaka huu.

Lindner ameongeza kuwa pamoja na mpango wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha, serikali itawasilisha azimio bungeni kuelezea hali ya kipekee ya dharura, hali ambayo ndio msingi wa kisheria wa kusimamisha sheria ya deni.

Soma pia:  Rungu la Mahakama latikisa sehemu ya bajeti ya Ujerumani

Wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Ujerumani ilisema kuwa serikali ya Kansela Olaf Scholz imevunja masharti ya katiba kwa kukiuka ibara inayoweka ukomo wa deni la taifa kupitia azma yake ya kuhamisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukabiliana na janga la Corona kwenda kwenye mfuko wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Uamuzi huo wa mahakama uliiacha serikali kuu na pengo la euro bilioni 60 katika bajeti yake na hivyo basi kutilia shaka uwezekano wa kuendelea na miradi ya maendeleo na uwekezaji.

Serikali yasitisha miradi mingi ya kimkakati

Kufuatia uamuzi huo, serikali imesitisha miradi mingi inayofadhiliwa kupitia mfuko wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuweka kizuizi kikubwa cha matumizi katika miezi iliyosalia ya mwaka huu 2023.

Olaf Scholz I Berlin I SPD
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Thomas Imo/photothek/picture alliance

Ibara hiyo ya katiba iliyoingizwa mwaka 2009 chini ya utawala wa aliyekuwa Kansela Angela Merkel, inapunguza ukopaji mpya katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya kwa hadi kiwango cha asilimia 0.35 ya pato jumla la taifa.

Sheria hiyo ilisitishwa kutoka mwaka 2020 hadi 2022 wakati wa janga la Corona na mzozo wa nishati, japo ilipangwa kuanza tena kutumika mwaka huu.

Usitishwaji wa sheria hiyo tata ya madeni itakuwa mwiba mkali kwa vyama washirika vya SPD, chama cha kijamii na chama cha kiliberali kinachoelemea biashara cha FDP.

Kusimamishwa kwa sheria hiyo ya deni ni pigo hasa kwa Lindner, ambaye amejijengea sifa juu ya usimamizi mzuri wa masuala ya fedha.

Katika mkutano na waandishi wa habari, waziri huyo wa fedha ambaye amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwekwa mipaka kwenye viwango vya madeni, aliepuka kutaja moja kwa moja uamuzi wa mahakama wa kusimamisha mipango ya matumizi ya serikali.

Soma pia: Scholz amtaka Putin kuvimaliza vita vya Ukraine 

Lindner badala yake ameeleza kuwa, atawasilisha bajeti mpya ya mwaka 2023 wiki ijayo ili "kusafisha njia” kabla ya kuanza kuzungumzia tena bajeti ya mwaka 2024 na miaka mingine ijayo.

Ameandika katika mtandao wake wa kijamii kuwa, "hakuna deni jipya litakalochukuliwa. Badala yake, fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya usimamizi wa matatizo ya dharura zitawekwa kwenye msingi wa kisheria."

Gazeti la kila wiki la Ujerumani la der Spiegel limeripoti kuwa bajeti ya ziada itakuwa na kiasi cha euro bilioni 40, na kufanya nakisi ya jumla ya Ujerumani mwaka huu hadi euro bilioni 85.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake