1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Merkel atoa mwito kwa Umoja wa Ulaya kuafikiana

16 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBrA

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,ametoa mwito kwa wanachama wote wa Umoja wa Ulaya kuwa tayari kuafikiana,akijaribu kupata makubaliano kuhusu katiba mpya ya umoja huo.Juma lijalo mjini Brussels katika mkutano wa kilele wa umoja huo, Merkel atawasilisha mswada wa katiba uliofanyiwa marekebisho.Merkel ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya,ametoa mwito huo katika ujumbe wake wa kila juma kwenye mtandao wa Internet.Amesema,ni matumani yake kuwa juma lijalo watafanikiwa kuidhinisha mswada huo na hivyo kuweka msingi wa kupata mkataba mpya na kuipa Ulaya tena uwezo wa kujadiliana.

Poland imetishia kuupinga mkataba huo,pindi hofu zake hazitozingatiwa kuhusika na mfumo wa upigaji kura uliopendekezwa.Merkel anatazamiwa kukutana na Rais Lech Kaczynski wa Poland baadae leo jioni karibu na jiji la Berlin.Mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya umekwama baada ya wapiga kura nchini Ufaransa na Uholanzi kuikataa katiba hiyo katika kura ya maoni iliyopigwa miaka miwili iliyopita.