1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter abadilisha mawazo kuhusu ubaguzi

5 Aprili 2013

Rais wa FIFA Sepp Blatter amelegeza msimamo wake kuhusiana na pendekezo la vilabu kushushwa daraja na kupokonywa pointi kama adhabu ya kupatikana na hatia ya ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/18Aiu
FILE - In this March 30, 2012 file picture FIFA President Sepp Blatter gestures during a press conference at the FIFA headquarters in Zurich, Switzerland. FIFA President Sepp Blatter defended his role in a World Cup kickbacks scandal on Thursday July 12, 2012, after his former boss Joao Havelange was formally identified for taking millions of dollars in payments from marketing deals. FIFA published a Swiss prosecutor's report on Wednesday confirming that Havelange accepted kickbacks in the 1990s during Blatter's 17-year stint serving him as FIFA's top administrator. Asked if he knew that Havelange took kickbacks from disgraced marketing agency ISL, Blatter said "commission" payments were legal in Switzerland in the 1990s. (AP Photo/Anja Niedringhaus,File)
FIFA Sepp Blatter in der KritikPicha: AP

Sasa Blatter amesema kua huenda ikawahimiza mashabiki kujaribu makusudi kushinikiza mechi kusitishwa. Mnamo Januari mwaka juu, Mswisi huyo mwenye umri wa miaka 77 alipendekeza uwezekano wa kuanzishwa vikwazo vya aina hiyo kwa timu ambazo mashabiki wake watapatikana na hatia ya ubaguzi wa rangi lakini sasa anaonekana kuulegeza msimamo huo katika hotuba yake aliyotoa katika hafla moja mjini Zurich jana Ijumaa. Blatter amewaambia waandishi habari kuwa ni lazima kitu kifanywe kuhusiana na suala hilo, lakini hatari ni kuwa kama watakubali mchuwano kurudiwa, au kuwepo na kupunguzwa pointi au chochote kile, hilo linaweza kufungua mlango kwa makundi ya wahuni kusababisha matatizo. Na ndiyo maana udhibiti wa viwanja unahitajika. Blatter amesema uamuzi huenda ukapatikana katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la FIFA mwezi Mei wa kutoa wito wa kuwepo vikwazo vya pamoja kote ulimwenguni.

Kwamba hatua za kinidhamu ni lazima zichukuliwe kote ulimwenguni, ni lazima ziwe katika kamati zote za kinidhamu, na mashirikisho pamoja na ligi na ni lazima ziwe za kiwango sawa.

Bayern ndio washindi?

Katika soka ya Ujerumani, Bundesliga ni kuwa mafanikio ya Bayern Munich, msimu huu bila shaka kwa kiasi umechangiwa na uwekezaji uliofanywa wa euro milioni 40 wa kumsajili Javi Martinez, mshambuliaji Mario Mandzukic na beki Dante. Bayern walimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita, katika Bundesliga, na Champions League na kufuatia uchungu wa kushindwa na Chelsea uwanjani mwao kupitia penalti katika fainali ya Champions League, Bayern walijizatiti kutwaa tena umahiri wa nyumbani na pia kujaribu kwa mara nyingine kutafuta ubingwa wa jukwaa la Ulaya. Mandzukic alifaulu kuvaa viatu vya Mario Gomez aliyekuwa na jeraha, katika safu ya mashambulizi, wakati beki Dante akiwa ngome imara katika safu ya ulinzi.

Bayern München wameandaa mvinyo kusheherekea ubingwa wao wa Bundesliga msimu huu wa 2012/13
Bayern München wameandaa mvinyo kusheherekea ubingwa wao wa Bundesliga msimu huu wa 2012/13Picha: REUTERS

Kocha Jupp Heynckes anaondoka mwishoni mwa msimu huu, na kumwachia mikoba mkufunzi mpya anayefahamika kote ulimwenguni na kumezewa mate Pep Guardiola. Na bila shaka wengi wanasubiri kuona mafanikio atakayoyaleta katika klabu hiyo tajiri Ujerumani,

Man United na Man City kuumana

Katika Ligi ya Soka England ambapo Manchester United wako kileleni na pengo la pointi 15 mbele ya Manchester City na wanaonekana kuendeleza rekodi ya mafanikio yao kwa kutwaa taji la 20 wakati zikisalia mechi nane pekee msimu kukamilika. United wataangushana na City Jumatatu hii uwanjani Old Trafford na kama watashinda basi United watapanua pengo lao hadi pointi 18 mbele ya watani wao wa karibu City kukisalia mechi saba pekee za kuchezwa.

Manchester United wanaonekana kuendeleza rekodi yao ya taji la 20 la Premier League, England
Manchester United wanaonekana kuendeleza rekodi yao ya taji la 20 la Premier League, EnglandPicha: Reuters

City wanaonekana kumaliza katika nafasi ya pili, lakini kinyang'anyiro cha nafasi za tatu na nne kinaendelea kuwa kikali na huenda kikaamuliwa katika mchuwano wa mwisho kabisa huku Tottenham ikicheza na City na Chelsea. Arsenal ni lazima wacheze na United na Everton. Kesho Jumapili, Chelsea v Sunderland, Liverpool v West Ham, Newcastle v Fulham, QPR v Wigan wakati Tottenham v Everton.

Afrika Kusini na FIFA wakubaliana

na kwingineko Afrika Kusini na Shirikisho la Soka ulimwenguni FIFA wamefaulu kutatua mgogoro uliokuwepo kuhusiana na uchunguzi wa nchi hiyo katika kashfa ya kupanga mechi kabla ya kuanza dimba la dunia dunia mwaka wa 2010. FIFA imesema kuwa mzozo huo umetatuliwa baada ya mazungumzo yaliyofanywa katika makao yake makuu nchini Uswisi baina ya waziri wa michezo wa Afrika kusini Fikile Mbalula na mkuu wa Shirikisho la soka Afrika Kusini Kirsten Nematandani.

FIFA imesema tume huru ya uchunguzi inaundwa na serikali ya Afrika Kusini kuchunguza madai hayo. Ripoti ya FIFA ilidai kuwa nne kati ya mechi nne za Afrika Kusini za kujupima nguvu kabla ya nchi hiyo kuandaa dimba la dunia, zilipangwa na marefarii wafisadi kutoka Kenya, Niger, na Togo.

Na kufikia hapo basi mpenzi wa michezo, ndipo nateremsha pazia kwa leo, kwa niaba ya wenzangu wote hapa nakutakia jioni njema. Mimi ni Bruce Amani kutoka Bonn, tukutane mara nyingine, kwaheri kwa sasa

Mwandishi: Bruce Amani/AD/Reuters/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef