1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BOUAKE : Waziri Mkuu wa Ivory Coast anusurika kuuwawa

29 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBnH

Waziri Mkuu wa Ivory Coast Guillaume Soro amenusurika kuuwawa wakati ndege yake iliposhambuliwa na roketi wakati ikiwasili katika ngome kuu ya waasi katika mji wa Bouake leo hii watu watatu wameuwawa kwenye shambulio hilo.

Soro kiongozi wa kikundi cha waasi cha New Forces kilioko kaskazini mwa nchi hiyo ambacho kiliteka eneo la kaskazini mwa nchi hiyo wakati wa vita vifupi vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002 hadi 2003 alitangazwa kuwa waziri mkuu hapo mwezi wa April baada ya kusaini makubaliano ya amani na Rais Laurent Gbagbo kuingoza nchi hiyo kwenye uchaguzi mkuu uliochelewa mno kuitishwa.

Allan Aliali mwandishi wa gazeti la chama cha Gbagbo la Notre Voie ambaye alikuwemo ndani ya ndege hiyo amesema ameshuhudia maiti tatu ndani ya ndege hiyo ambazo hakuweza kuzitambuwa.

Soro baadae alionekana akiwasili kwenye makao makuu ya waasi hao mjini humo bila ya majeraha juu ya kwamba wajumbe wengine wa msafara wake walikuwa na majeraha ya wazi.