1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BREMEN: Mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya wakutana

30 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCE1

Kiongozi wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, ameileza hatua ya Iran kuwazuilia wanamaji 15 wa Uingereza kuwa kosa kubwa. Solana amewaambia waandishi wa habari mjini Bremen kaskazini mwa Ujerumani kwamba Iran inatakiwa iwaachilie wanajeshi hao haraka bila masharti yoyote.

´Ninahakika kwamba mashua ya wanamaji wa Uingereza lilikuwa katika eneo la bahari ya Irak. Na hata iweje, la muhimu ni Iran iwaachilie huru wanajeshi hao mara moja bila masharti yoyote.´

Akihudhuria mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya mjini Bremen Ujerumani, waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, Margaret Beckett, amewambia waandishi wa habari kwamba hakuna dalili za Iran kujaribu kuutanzua mzozo huo kwa haraka. Hata hivyo anatumai Umoja wa Ulaya utatoa taarifa ya pamoja hii leo kuiunga mkono Uingereza.

´Tunachohisi ni kwamba wenzetu wa Umoja wa Ulaya wanaelewa hali halisi ilivyo na wanatusadia na kutuunga mkono hasa Ujerumani ambayo ni rais wa umoja huo. Tunashukuru kwa hilo na tuna matumaini bila shaka taarifa ya pamoja itatolewa na umoja wa Ulaya hii leo.´

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Bremen kujadili maswala kadhaa ikiwa ni pamoja na mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Mwenyekti wa mazungumzo ja mjini Bremen ambayo si rasmi, ni waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinemer, ambaye nchi yake ni rais wa Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa umoja huo wataamua juu ya swala la kuwa na mahusiano na serikali mpya ya umoja wa kitaifa ya mamlaka ya Palestina.