1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Umoja wa Ulaya waishambulia Uturuki juu ya mageuzi

8 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCuo

Tume ya Umoja wa Ulaya leo hii imeionya Uturuki kuharakisha mageuzi ya kisiasa yanayozorota na kudai kufunguliwa mara moja na kwa ukamilifu kwa viwanja vya ndege na bandari za Uturuki kwa meli za Cyprus ya asili ya Ugiriki.

Katika repoti juu ya maendeleo yaliofikiwa na Uturuki katika kutimiza masharti ya uwanachama wa Umoja wa Ulaya tume hiyo ambacho ni kitengo kikuu cha utendaji cha Umoja wa Ulaya imeweka wazi kwamba serikali ya Uturuki bado ina njia ndefu ya kwenda kabla ya kutimiza kanuni za Umoja wa Ulaya.

Repoti hiyo imetolewa leo hii mjini Brussels na Kamishna anayeshughulikia masuala ya kutanuka kwa Umoja wa Ulaya Olli Rehn.

Kwa mujibu wa maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya Uturuki imepewa hadi kati kati ya mwezi wa Desemba kutekeleza mkataba muhimu wa forodha na nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya Cyprus ya asili ya Ugiriki au venginevyo nchi hiyo inaweza kukabiliwa na kusitishwa kwa mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo repoti hiyo haikutowa mapendekezo ya wazi iwapo mazungumzo hayo yasitishwe na imeliwachia suala hilo liamuliwe na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao wa kilele hapo mwezi wa Desemba.