1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUJUMBURA : Msuluhishi kukwamua mchakato wa amani

13 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC2g

Msuluhishi wa Afrika Kusini amewasili mjini Bujumbura hapo jana kuendeleza mbele machakato wa amani uliokwama kati ya serikali na kundi la waasi lililobakia nchini humo la FNL.

Kundi la FNL lilijitowa katika timu ya kusimamia usitishaji wa mapigano mwezi uliopita kwa kusema kwamba wanajeshi wa serikali hawakuondoka kwenye maeneo yalioko chini ya udhibiti wao ambalo ni mojawapo ya masharti ya suluhu yaliotiwa saini mwezi wa Septemba.

Juu ya kwamba pande zote mbili zimesema kwamba ziko tayari kwa mazunguzo bado hazikukubaliana juu ya wakati wa kuanza mazungumzo hayo na mahala pa kufanyika.

Msuluhishi huyo wa Afrika Kusini Charles Ngakula ambaye amekuwa na mazungumzo na Rais Piere Nkurunziza wa Burundi amesema yuko nchini humo kuangalia jinsi ya kuondowa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa usitishaji wa mapigano.

Ngakula amesema anapanga kwenda Dar es Salaam Tanzania kukutana na viongozi wa FNL na kutowa repoti kwa viongozi wa kanda ambao ndio watakaoamuwa tarahe na mahala pa mkutano.