1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAIRO: Abbas aungwa mkono na mawaziri wa nje wa Kiarabu

16 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBrF

Mawaziri wa masuala ya nje wa nchi za Kiarabu wameahidi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas, baada ya wanamgambo wa kundi la Hamas kudhibiti Ukanda wa Gaza.Kwenye mkutano wa dharura wa Umoja wa Nchi za Kiarabu mjini Cairo,mawaziri hao pia waliamua kuunda kamati itakayochunguza mgogoro kati ya Hamas na chama cha Fatah cha Rais Abbas.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu,Amr Moussa ametoa mwito kwa Wapalestina kusitisha mapigano yao.Amesema, wao kama kundi la Waarabu,hawawezi kuikubali hali iliyoshuhudiwa Gaza.Akaongezea,pindi hali hiyo itarudiwa basi kutakuwepo msimamo mwingine.

Wakati huo huo mjini Ramallah mpango wa kutaka kuiapisha serikali mpya ya mpito umeahirishwa bila ya kutoa sababu.Rais Abbas ameivunja serikali ya umoja na amemchagua mwanasiasa asie na chama,Salam Fayad kuiongoza serikali mpya ya mpito,baada ya kumfukuza waziri mkuu Ismail Haniyeh wa Hamas.Hatua hiyo inapingwa vikali na chama cha Hamas.Chama cha Fatah kimekataa mwito wa Hamas wa kufanya kazi pamoja.

Kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu,si chini ya watu 116 wameuawa katika mapigano ya juma moja kati ya makundi hasimu ya Hamas na Fatah.