1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CONMEBOL taabani kutokana na rushwa

4 Desemba 2015

Kukamatwa kwa marais watatu wa mwisho wa CONMEBOL kumelitumbukiza Shirikisho hilo la Kandanda la Amerika Kusini katika mgogoro mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa barani humo katika historia ya miaka 100

https://p.dw.com/p/1HHa7
Paraguay Luque Conmebol Conventions Center
Picha: picture-alliance/epa/A. Christaldo

Bara hilo ambalo ni makao ya miamba wa kandanda kama vile Argentina na Brazil na baadhi ya wachezaji bora zaidi katika sayari hii linakabiliwa na kibarua kikali cha kurejesha uadilifu wake na uthabiti baada ya kutumbukia katika kashfa kubwa ya kandanda la dunia. Rais wa CONMEBOL Juan Angel Napout alikamatwa Alhamisi katika msako uliofanywa kwenye hoteli moja ya kifahari nchini Uswisi kama sehemu kesi pana ya rushwa inayolihusisha shirikisho la kandanda la Kimataifa – FIFA ambayo inaendeshwa na Wizara ya Sheria ya Marekani.

Napout, ambaye pia ni makamu wa rais wa FIFA anapinga kuhamishwa kwake nchini Marekani. Ni miongoni mwa watu 16 wanaotuhumiwa kwa mashtaka ya rushwa kama sehemu ya uchunguzi wa waendesha mashtaka wa Marekani.

Miongoni mwa maafisa wengine wa Amerika Kusini walioshtakiwa ni Ricardo Teixeira, mkuu wa zamani wa shirikisho la kandanda la Brazil, Marco Polo del Nero, rais wa Shirikisho la kandand la Brazil, Katibu Mkuu wa CONMEBOL ambaye alijiuzulu hivi karibuni Jose Luis Meiszner, Manuel Burga rais wa zamani wa shirikisho la kandanda la Peru na Luis Chiriboga, rais wa shirikisho la kandanda la Equador.

USA, Loretta Lynch
Picha: picture-alliance/dpa/M. Reynolds

Mwingine ni Carloz Chavez, mwekahazina wa zamani wa CONMEBOL na rais wa shirikisho la kandanda la Bolivia ambaye alifungwa jela mwmezi Julai kutokana na mashtaka ya uchunguzi tofauti wa rushwa.

Mkurugenzi mkuu wa CONMEBOL Gorka Villar, amesema wataendelea kujitahidi kurekebisha hali katika shirikisho hilo. "Naamini kuwa maafisa wa shirikisho la kandanda la Amerika Kusini wanafanya kazi. Wanajaribu kutimiza malengi ambayo yaliwekwa baada ya hali hii yote kutokea. Naamini wanafanya kazi vyema lakini kwa wakati huu tunayaimarisha malengo yetu katika mwaka ambao haujawa rahisi – lakini unatoa mafanikio".

Akitihibitisha kukamatwa kwa maafisa wapya wa FIFA pamoja na kufunguliwa mashtaka mapya, mwendesha mashtaka wa Marekani Loretta Lynch alisema hakuna yeyote atakayekwepa uchunguzi wao. "Sasa acha niseme kuwa usaliti wa haki ambao umeonekana hapa ni wa kikatili na kiwango cha rushwa kilichodhihirika hapa hakikubaliki kabisa na ujumbe unaotoka kwa tangazo hili unapaswa kuwa wazi kabisa kwa kila mmoja anayehusika, ambaye angali mafichoni na anatumai kukwepa uchunguzi unaoendelea, hautangoja tumalize na hautakwepa uchunguzi wetu. Pia natangaza kuwa wengi wametii onyo letu. Watu nane zaidi wamekubali kukiri mashtaka ya kuhusika kwao katika mipango cha ufisadi ambayo tumeiangazia".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo