1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Kusawazisha uhusiano na Saudi Arabia ni kipengele

18 Januari 2024

Rais wa Israel Isaac Herzog amesema kusawazisha uhusiano na Saudi Arabia ni kipengele muhimu cha kumaliza vita na Hamas na kwa mabadiliko katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4bQXB
Jukwaa la Kiuchumi la Davos | Rais wa Israel Isaac Herzog akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani  Antony Blinken
Rais wa Israel Isaac Herzog akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Abir Sultan/AFP/Getty Images

Herzog ameyasema hayo katika mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la kimataifa la kiuchumi, unaofanyika katika mji wa mapunziko wa Davos nchini Uswisi.

Kauli hiyo ya Rais wa Israel imekuja siku chache baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan, kusema mjini Davos kwamba taifa hilo la Kifalme linakubali kuwa amani ya kikanda inaihusisha Israel, na kwamba Saudi Arabia itaitambua nchi hiyo pasina shaka, kama sehemu ya makubaliano mapana ya kisiasa.

Lakini Mwanamfalme bin Farhan aliongeza kuwa hilo linaweza tu kutokea kupitia amani ya Wapalestina, kupitia kuundwa kwa taifa la Wapalestina.

Rais Herzog amesema suala hilo ni gumu na litachukuwa muda mrefu, lakini ameongeza kuwa ni fursa kwao kusonga mbele duniani na katika kanda kuelekea mustakabali bora.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinkenpia alisisitiza katika mazungumzo mjini Davos kwamba njia ya kupatikana kwa taifa la Palestina inaweza kusaidia kuboresha usalama wa Israel na uhusiano wake na mataifa mengine katika kanda.

Waziri Mkuu wa Israel na serikali yake ya mrengo mkali wa kulia hata hivyo, wanapinga dhana ya suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo wa Israel na Wapalestina.

Soma pia:Rais wa Israel Herzog ahudhuria Kongamano la Kiuchumi Davos, Uswisi

Herzog pia ametumia jukwaa hilo la kimataifa kusisitiza athari za kidunia la shambulio la Hamas la Oktoba 7, ambalo amesema ni moja tu ya mawakala wa kile alichokitaja kama "himaya ya uovu inayoanzia Tehran.

"Una Hezbollah upande wa Kaskazini, inayopatiwa silaha na kufadhiliwa na Iran, na wanafyatua tu makombora na kuua raia, wanajeshi na kuingia vitani na Israel." Alisema rais wa Israel katika mkutano wa Davos

Aliwakumbusha viongozi wa ulimwengu kwamba, dunia ina kawaida ya kusahauna wakati unakwenda. Lakini ukweli ni kwamba Israel inapigana vita kwa ajili ya ulimwengu mzima, ulimwengu huru

"Hivyo vita hivi ni kipengele muhimu katika historia ya wanadamu." Alisisitiza Herzog

Hatua za Iran dhidi ya oparesheni za Israel

Katikati mwa mzozo wa kivita wa Gaza, Iran imechukuwa hatua za kijeshi dhidi ya kile inachokiita operesheni za intelijensia za Israel katika taifa jirani la Iraq.

Waasi wa Kihouthi nchini Yemen wanaoungwa mkono na Iran, pia wameongeza mashambulizi dhidi ya meli za mizigo katika bahari ya Shamu, na kusababisha mkururo wa mashambulizi ya kujibu kutoka kwa Marekani na Uingereza.

Davos, Uswisi | Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hussein Amirabdollahian
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hussein Amirabdollahian akizungumza katika Jukwaa la Kiuchumi la Dunia WEF, mjini Davos, Uswisi.Picha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Herzog amesema suala la Wahouthi ndiyo kipaumbele chao cha kwanza, kwa sababu linapandisha gharama ya maisha ya kila familia duniani.

Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Siku ya Jumatano, waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amiraddollahiano, alisisitiza kuwa mashamulizi ya Iran nchini Iraq, dhidi ya kilichodaiwa kuwa kambi ya wanamgambo nchini Pakistan, yalikuwa sehemu ya haki ya nchi yake kujilinda, na kuishtumu Israel kwa mauaji ya kimbari katika kampeni yake dhidi ya Hamas, ambayo imesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia wa Kipalestina.

Rais wa Israel, amekuwa mojawapo wa viongozi waliozungumza leo katika mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi, WEF, ulioko katika siku yake ya tatu leo, pamoja na waziri mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, Waziri wa Fedha Qatar Ali Al Kuwari  na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya OpenAI Sam Altaman.

Mkutano huo wa siku nne unajadili mada kadhaa, zikiwemo wasiwasi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na teknolojia ya akili ya kubuni, ambayo inatoa ahadi ya kiuchumi kwa baadhi na hatari kubwa kwa wengine.

Kwanini Afrika Kusini inaishtaki Israel ICJ?