1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England yahitaji muujiza baada ya kuchapwa na Uruguay

20 Juni 2014

Luis Suarez alitikisa wavu mara mbili wakati Uruguay ikiwaduwaza England kwa kuwapa kipigo cha magoli mawili kwa moja katika mechi kali iliyojawa na hisia nyingi. England wanastahili muujiza kufuzu katika duru ya pili

https://p.dw.com/p/1CMZh
Fifa WM 2014 Uruguay England
Picha: Getty Images

Mshambuliaji huyo wa Liverpool Suarez alifunga magoli mawili ya wizi na la pili lilikuja katika dakika ya 85, ya mchuano huo wa kundi D mjini Sao Paulo baada ya Wayne Rooney kuonekana kuwapa England pointi moja kupitia bao lake la kusawazisha katika dakika ya 75.

Kichapo hicho kimewaacha England, ambao walizabwa magoli mawili kwa moja na ITALIA katika mechi yao ya ufunguzi, wakihitaji muujiza ili waepuke fedheha ya kushindwa kufuzu katika duru ya pili ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1958. Kocha wa England Roy Hodgson alisema wamefedheheka sana na kuvunjwa moyo baada ya matokeo hayo.

Fifa WM 2014 Uruguay England
Luis Suarez alikuwa mwiba katika lango la EnglandPicha: Getty Images

Suarez ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka nchini England baada ya kuwa na msimu wa kusisimua, alikuwa ametiliwa shaka kucheza Kombe la Dunia baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwezi Mei. Hata hivyo mshambuliaji huyo mwenye umti wa miaka 27 alirejea tena kuiandamana timu ya England iliyokuwa na wachezaji watano anaocheza nao katika klabu ya Liverpool.

Huku timu zote zikifahamu wazi kuwa kichapo kingeyauwa matumaini yao ya kufuzu katika duru ya 16 za mwisho, mechi hiyo ilianza kwa tahadhari kubwa. Baada ya nahodha wa England Steven Gerrard kuupoteza mpira, Uruguay walifanya shambulizi kupitia mchezaji Nicolas Lodeiro aliyemsukumia pasi Edinson Cavani ambaye alichonga krosi safi iliyomfikia Luis Suarez na akamalizia kwa kichwa hadi ndani ya wavu.

Lakini dakika 15 kabla ya mechi kukamilika, Rooney alifunga bao lake la 40 la kimataifa, na lake la kwanza kabisa katika Kombe la Dunia, baada ya kuandaliwa pasi na Glen Johnson. England ilionekana kuwa ingefunga goli jingine, lakini dakika tano kabla ya mchezo kukamilika, mpira ulimfikia Suarez baada ya Gerrard kufanya kosa katikati ya uwanja, na mshambuliaji huyo akatimka mbio kuelekea kwenye lango ambapo alisukuma kombora kali hadi ndani ya nyavu.

Ushindi wa Uruguay una maana kuwa England itaoma Italia izishinde Costa Rica hii leo Ijumaa, na Uruguay Jumanne wiki ijayo. England kisha itahitaji kupata ushindi dhidi ya Costa Rica katika mchuano wake wa mwisho ili kwua na nafasi yoyote ya kufuzu kwa tofauti ya magoli.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo