1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eritrea imepunguza msaada wake kwa al-Shabaab

17 Julai 2012

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa imesema Eritrea imepunguza msaada wake kwa kundi la wanamgambo wa al-Shabaab nchini Somalia kutokana na shinikizo la kimataifa, lakini bado inakiuka maazimio ya Baraza la Usalama

https://p.dw.com/p/15YpJ
Pro-Palästina Demonstration der Al-Shabaab Miliz in Somalia
Symbolbild Islamisten Kenia SomaliaPicha: picture-alliance/Photoshot

Kundi la Uangalizi la Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia na Eritrea, ambalo linachunguza ukiukaji wa vikwazo vya silaha dhidi ya nchi hizo mbili, limesema katika ripoti yake lililowasilisha kwa Baraza la Usalama kuwa halikupata ushahidi wa msaada wa moja kwa moja wa Eritrea kwa al-Shabaab katika kipindi cha mwaka uliopita.

Ripoti hiyo inasema ijapokuwa inawezekana kuwa maafisa wa Eritrea wanaendelea kutoa usaidizi wa kifedha na mbinu nyingine za msaada kwa makundi ya upinzani nchini Somalia, bila shughuli zao kugundulika, kundi la Uangalizi linatathmini kuwa usaidizi wa aina yoyote kama huo ni mdogo.

Mji wa Mogadishu umeshuhudia mashambulizi mengi ya wanamgambo wa kujitoa mhanga
Mji wa Mogadishu umeshuhudia mashambulizi mengi ya wanamgambo wa kujitoa mhangaPicha: Reuters

Badala yake jopo hilo liliwasilisha ushahidi kuwa Eritrea iliwatuma waasi wa Ethiopia kupitia Somalia, ikayauzia makundi haramu silaha nchini Sudan ambayo hufanya biashara na wafanyabiashara wa silaha wa Palestina na ikaagiza kutoka ng'ambo vipuri vya jeshi lake la angani.

Aidha ripoti hiyo ilidai kuwa waasi wa kabila la Afar waliohusika na mauaji ya watalii watano wa Ulaya Kaskazini mwa Ethiopia mwezi wa Januari mwaka huu walipewa hifadhi na mafunzo nchini Eritrea, ijapokuwa hakukuwa na ushahidi kuwa nchi hiyo ya bahari ya shamu ilikuwa na jukumu la moja kwa moja katika mauaji hayo.

Iliishutumu Eritrea kwa kukataa kukubaliana na maazimio ya Baraza la Usalama na inaendelea kuwa na ushawishi mbaya na kufanya uharibifu katika kanda hiyo.

Nchi hiyo awali imekanusha madai hayo na ikatoa wito wa kubadilishwa wanachama wa jopo hilo kuhusu kile inakiita kuwa ni wanaipendelea Ethiopia ambayo ni hasimu wake mkuu. Wajumbe wa Eritrea katika Umoja wa Afrika walikataa kuzungumzia ripoti hii ya Umoja wa Mataifa.

Kanisa la African Inland lililoshambuliwa kwa gurunedi mjini Garissa
Kanisa la African Inland lililoshambuliwa kwa gurunedi mjini GarissaPicha: Reuters

Wakati huo huo Umoja wa Afrika –AU umelitaja shambulizi la bomu nchini Somalia ambalo lilisababisha kifo cha mbunge mmoja na kuwajeruhi watu watano kuwa ni kitendo cha “uwoga” kilicholenga kuhujumu mchakato wa amani katika nchi hiyo inayokumbwa na vita.

Mohamed Abdinur Garweyne aliuawa katika mripuko huo uliotokea mjini Mogadishu, ambao kundi la al-Shabaab lilikiri kuhusika.

Kwingineko polisi watatu wa Kenya wameuawa katika shambulizi lililofanywa Kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Somalia jana Jumatatu.

Kenya imekumbwa na msururu wa mashambulizi ya gurunedi na mabomu tangu vikosi vyake vilipovuka mpaka na kuingia nchini Somalia mwezi Oktoba mwaka jana na imelilaumu kundi la al-Shabaab, na wale wanaoliunga mkono kundi hilo ndani ya Somalia. Mkuu wa polisi wa jimbo la Garissa George Kingi alisema Polisi hao watatu waliuawa wakiwa safarini kuelekea eneo la Liboi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Josephat Charo