1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fainali ya soka ya mataifa ya Afrika

Mohamed Abdulrahman6 Februari 2015

Macho na masikio ya mashabiki wa soka barani Afrika na hata nje ya bara hilo, Jumapili yataelekezwa nchini Guinea ya Ikweta katika pambano hilo la fainali kati ya Cote d´Ivoire itaumana na Ghana

https://p.dw.com/p/1EWP1
Afrika Cup 2015 Tunesien – Äquatorialguinea
Mchuano wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2015, Tunisia na Guinea ya IkwetaPicha: AFP/Getty Images/K. Desouki

Katika mchuano wa fainali ya kombe la kandanda la mataifa ya Afrika. Cote d´Ivoire ilifanikiwa kuingia fainali baada ya kuibwaga Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 3-1 Jumatano na hapo alhamisi katika nusu fainali nyingine Ghana nayo ikawalaza wenyeji guinea ya Ikweta mabao 3-0. Hata hivyo pambano hilo lilikumbwa na machafuko ya mashabiki wa Guinea ya Ikweta walioanza kuwashambulia kwa chupa za maji mashabiki wa Ghana walioingiwa na hofu na kulazimika kukimbilia nyuma ya lango uwanjani kujinusuru. Ilikuwa ni baada ya kupachikwa bao la tatu na mchezo kusimamishwa katika dakika ya 82 kwa zaidi ya dakika 35, huku wachezaji wa timu zote mbili wakitafuta hifadhi katikati ya uwanja. Polisi wa kuzuwia fujo walitumia virungu na gesi ya kutoa machozi kuzuwia ghasia. Kocha wa Guinea ya Ikweta Esteban Becker ameungaman kwamba amehuzunishwa na kitendo hicho na nyota wa Ghana Andre Ayew alielezea kukasirishwa kwake na ghasia hizo. Guinea ya Ikweta ambayo haikutarajiwa kufika nusu fainali, itaumana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo leo kuwania nafasi ya tatu .Lakini haikuweza kufahamika mapema kama mechi hiyo itachezwa katika uwanja huo huo mjini Malabo . Kwa upande mwengine fainali ya kombe hilo la mataifa ya Afrika kesho jumapili kati ya Cote d´Ivoire na ghana katika uwanja wa mji wa bandari wa Bata, itakuwa ni marudio ya fainali ya 1992 mjini Dakar Senegal,ambapo Cote d´Ivoire ilishinda kwa penalti, kwa mikwaju 11 dhidi ya 10, baada ya dakika 120 kushindwa kutoa mshindi na timu hizo kubakia sare bila kwa bila.

Bundesliga:

Katika ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, Borussia Dortmund inaendelea kukumbwa na msukosuko baada ya kujikuta ikikamata mkia katika mtazamo wa ligi hiyo ilipofungwa na Augsburg bao moja kwa bila Jumatano, licha ya Augsburg kujikuta ikicheza sehemu kubwa ya sehemu ya mwisho ya pambano hilo ikiwa na wachezaji 10 baada ya Christoph Janker kupewa adhabu ya kadi nyekundu kwa kumkwatua Pierre-Emerick Aubameyang. Pigo hilo lilikuwa la 11 msimu huu na kuiacha kilabu hiyo ya Kocha Juergen Klopp ikiwa nafasi ya mwisho, akiwa na pointi 16 kutokana na mechi 19, matokeo anayompa mtihani mgumu kocha huyo.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - FC Augsburg
Borussia Dortmund ilipochuana na FC AugsburgPicha: Bongarts/Getty Images/A. Grimm

Kwa upande mwengine ,Michuano ya 20 ya ligi kuu ya Ujerumani Jumamosi ni kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich itakayokaribishwa na Stuttgart. Bayern inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 8 zaidi ya Wolfsburg inayoshika nafasi ya pili na ambayo itaumana leo na Hoffenheim, Freiburg inacheza nyumbani dhidi ya wageni Borussia Dortmund, Wolfsburg itachuana na Hoffenheim, Hamburg dhidi ya Hannover 96, Mainz 05 dhidi ya Hertha Berlin, wakati FC Köln watakua nyumbani kutoana jasho na SC Paderborn.

Wakati Bundesliga ikiendelea mwishoni mwa juma, Wolfsburg imekuwa timu iliotumia fedha nyingi zaidi katika zoezi la usajili katika kipindi cha majira ya baridi katika Bundesliga kuliko timu nyengine 17 za ligi hiyo kuu. Muda wa mwisho wa usajili ulipomalizika Jumatatu wiki hii ikathibitika kwamba Wolfsburg inamsajili Andre Schuerrle kutoka Chelsea kwa kitita cha euro zipatazo milioni 36.2 kwa wingi huyo mwenyeb umri wa miaka 24.

Kutokana na kumsajili pia Mchina Zhang Xizhe na mlinda mlango mbeligiji Koen Casteels kipindi hicho kwa kitita cha dola milioni 1.5 kwa kila mmoja wao, mabingwa hao wa Ujerumani mwaka 2009, ndiyo watumiaji kitita kikubwa cha fedha katika Bundesliga Ni zaidi ya euro milioni 60 zilizotumiwa na vilabu 18 katika msimu wa usajili na kufunja rekodi yausajili mwezi Januari ya msimu wa 2010-2011 ambapo zilitumika jumla ya euro milioni 50. Wolfsburg pia iliwapa uhuru wachezaji 50 kuondoka, wengi wao wakihamishwa kwa makubaliano ya mkopo. Pamoja na hayo rekodi ya kitita kikubwa cha fedha kwa jumla katika ligi kuu ya Ujerumani inashikiliwa na Bayern Munich, wakati ilipomsajili mlinzi wa kati, Mhispania Javi Martinez kwa kitita cha euro milioni 40.

Lattek afariki dunia:

Mashabiki wa kandanda nchini Ujerumani walipokea taarifa ya msiba wiki hii. Kifo cha mmoja wa makocha waliosifika Udo Lattek ambaye alishinda kombe la vilabu bingwa la Ulaya, lile la Shirikisho la kandanda barani Ulaya-Uefa na kombe la washindi akiwa na kilabu tatu tofauti. Lattek alifariki duniani Jumatano akiwa na umri wa miaka 80.Lattek aliiongoza Bayrern Munich kunyakuwa ubingwa wa Ulaya 1974 na ubingwa wa ligi kuu ya Ujerumani mara tatu baina ya 1972 na 1974. Baadae akachukuwa uongozi wa kuwa mkufunzi wa Borussia Monchengladbach na kushinda kombe la UEFA 1979 na ubingwa wa Ujerumani 1976 na 1977 kabla ya kuhamia uhispania alikoshinda kombe la washindi barani ulaya akiwa na Barcelona 1982. Kwa jumla Lattek alishinda mataji 14 na kilabu tatu na pamoja na mtaliani Giovanni Trapattoni , ndiyo makacha pekee walioshinda mataji yote matatu makubwa ya Ulaya. Miongoni mwa waliotuma salamu za rambi rambi ni pamoja na Rais wa Shirikisho la kandanda la kimataifa Sepp Blatter aliyesema , “Ni huzuni kubwa kwamba Udo lattek amefariki.”Udo Lattek ameacha mke na watoto wawili wa kike. Naye Rais wa Shirikisho la Kandanda la Ujerumani DFB, Wolfgang Niersbach, alitoa rambi rambi kwa niaba ya jamii ya michezo nchini Ujerumani.

Udo Lattek mit Diego Armando Maradona
Udo Lattek akiwa na Diego Armando MaradonaPicha: imago/Sven Simon

Kinyanganyiro cha Rais wa FIFA chapamba moto :

Makamu wa rais wa Shirikisho la kandanda duniani FIFA mwanamfalme wa Jordan Ali bin al-Hussein amesema jumahili kwamba , Marekani ni miongoni mwa vyama vya kitaifa kumteua kugombea kiti cha urais wa Shirikisho hilo dhidi ya Sepp Blatter mwenye umri wa miaka 78 na anayegombea kwa mara ya tano wadhifa huo wa kipindi cha miaka minne. Mwanamfalme huyo wa Jordan pia amefichua kwamba amethibitishwa na shirikisho la kandanda nchini mwake, Belarus, Malta, Uingereza na Georgia. Katika kampeni yake iliyozinduliwa mjini London , mwanamfalme huyo amesema , kuna utamaduni kiasi wa kutishana ndani ya FIFA, lakini ameongeza kuwa yeye anagombea kwa ajili ya dunia nzima.Lakini inaonesha kuna kazi ngumu anayokabiliana nayo kumuondoa Blatter madarakani, kiongozi ambaye anayegombea kwa mara ya tano, akiwania kipindi cha uongozi cha miaka mengine minne mwezi wa Mei. Michael van Praag wa Uholanzi na Luis Figo wa Ureno pia wamo katika kinyanganyiro hicho.

Riadha:

Mwanariadha bingwa wa olimpik ya walemavu aliyeko gerezani nchini Afrika kusini Oscar Pistorius amepokonywa shahada ya juu ya heshima aliyotunzwa na Chuo ikuu cha Strathclyde cha Uingereza 2012. Uamuzi huo ulitangazwa na taasisi hiyo ilioko Scotland wiki hii. Taarifa ilisema uamuzi huo unatokanan na kupatikana na hatia kwa mwanariadha huyo ya kuuwa bila ya kutegemea. Pistorius anatumikia kifungo cha miaka 5 jela kwa kumuuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp mnamo siku ya wapendanao-Valantines day- mjini Johannesburg mwaka 2013, na kusema alifikiria ni mwizi aliyeingia nyumbani kwake. Upande wa mashtaka ulidai alimuuwa makusudi, hoja ambayo ilikataliwa na jaji wa mahakama.

Pistorius aliweka historia alipotokeza kuwa mwanariadha wa kwanza kukimbia katika michezo ya Olimpik na ile ya Olimpik ya walemavu 2012 akitumia miguu ya bandia. Pistorius bingwa mara sita wa michezo ya olimpik ya walemavu alikatwa miguu yote miwili alipokuwa na umri wa miaka 11 kwa sababu ya hitilafu.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman