1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA: Kundi la Hamas laishambulia Israel

24 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7d

Kitengo cha kijeshi cha chama cha Hamas, Izz el—Deen al –Qassam, kimesema leo kwamba kimefanya mashambulio ya maroketi dhidi ya Israel kulipiza kisasi mashambulio ya Israel dhidi ya Wapalestina.

Maroketi 30 na makombora 60 yamevurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi mitano ya utulivu kulenga Waisraeli na kambi za jeshi.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema maroketi matano yamevurumishwa nchini Israel na mawili yameanguka karibu na mji ulio kusini mwa nchi hiyo.

Helikopta za Israel zimefyatua risasi kwenye waya wa sing´eng´e wa mpakani kusini mwa Ukanda wa Gaza katika juhudi za kuzuia maroketi hayo.

Naibu waziri mkuu wa Israel, Shimon Peres, amesema leo kwamba chama cha Hamas kimeshindwa kutimiza ahadi yake ya kusitisha mapigano.

Chama cha Hamas kimekanusha kufanya mashambulio yoyote ya maroketi dhidi ya Israel. Hata hivyo mwezi uliopita kilikubali kuhusika na mashambulio ya risasi na makombora katika kituo cha mpakani huko Gaza.