1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA : Rais Abbas akubali baraza la mawaziri

15 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIk

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina leo hii amekubali orodha ya baraza la mawaziri iliopendekezwa na Waziri Mkuu mteule Ismail Haniyeh wa kundi la Hamas na hiyo kufunguwa njia ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo inaweza ikakomesha umwagaji damu baina ya makundi ya Kipalestina.

Haniyeh amewaambia waandishi wa habari kwamba orodha ya baraza hilo la mawaziri itawasilishwa katika kikao maalum cha bunge kwa ajili ya kupigiwa kura ya kuidhinishwa hapo Jumamosi na linategemewa kuapishwa jioni hiyo.

Israel imesema itaisusia serikali hiyo mpya kama ilivyofanya kwa serikali iliopita iliokuwa ikiongozwa na Hamas kwa sababu ya kutolitambuwa taifa la Kiyahudi,kukataa kukanusha matumizi ya nguvu na kugoma kukubali makubaliano ya amani yaliopita kati ya Israel na Wapalestina kama inavyodaiwa na Umoja wa Ulaya na Kundi la Pande Nne linaloshughulikia amani ya Mashariki ya Kati.

Vikwazo vya kifedha vya kimataifa viliwekwa dhidi ya serikali iliokuwa ikiongozwa na Hamas baada ya kundi hilo la wanamgambo kushida uchaguzi wa Palestina mwaka jana.