1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gbagbo, kudhibiti usafirishaji wa Cocoa

Halima Nyanza8 Machi 2011

Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo ameitaka serikali yake kuchukua udhibiti wa uuzaji na usafirishaji wa zao la Cocoa wakati bado nchini humo kukiwa hakuna dalili zozote za kupungua kwa ghasia.

https://p.dw.com/p/10V6s
Rais Laurent GbagboPicha: AP

Akitangaza katika televisheni ya nchi hiyo, Laurent Gbagbo, Rais anayeng'ang'ania madarakani nchini Cote d'Ivoire amesema serikali kwa sasa, ndio itakayoidhinisha uuzaji ama ununuzi wa kahawa na Cocoa, mazao ambayo yanaongoza kusafirishwa nje ya nchi na yenye kuleta fedha nyingi za kigeni.

Hatua hiyo ya kutaifisha sekta za mazao hayo, imekuja wakati vikwazo vya fedha alivyoekewa Rais Gbagbo ambaye anang'ang'ania madarakani vimeanza kufanya kazi.

Lakini hata hivyo bado haijafahamika kutaifishwa kwa sekta hiyo kutaisaidia vipi serikali ya bwana Gbagbo.

Januari mwaka huu, mpinzani wa Gbagbo Alassane Ouattara, ambaye anaungwa mkono kimataifa aliwataka wafanyabiashara wa zao la Cocoa kuacha kusafirisha nje zao hilo katika jaribio la kutaka kuzuia faida anayoipata Gbagbo na kumzuia pia kuwalipa wafuasi wake.

Wakati hali ikiwa bado tete nchini humo, balozi wake mjini Washington Daouda Diabate, ameitaka Marekani kuisaidia nchi hiyo na watu wake.

Balozi Diabate, ambaye ameteuliwa na Ouattara ameyasema hayo baada ya  Ikulu ya Marekani kutangaza msaada wa dola milioni 12.6 kwa ajili ya wakimbizi na watu wengine wasio na makaazi nchini humo.

Akijibu swali kwamba Bwana Ouattara atakubali juu ya uwezekano wa kutumika kwa nguvu za kijeshi kumuondoa Bwana Gbagbo madarakani, Balozi huyo wa Cote d'Ivoire nchini Marekani alisema iwapo njia ya majadiliano itashindikana watatumia nguvu za kijeshi.

Aidha ametaka pia kuimarishwa kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo, kwa kusema kwamba jeshi la kulinda amani la umoja huo halina mamlaka yoyote nchini humo.

Umoja wa Afrika unasubiri jibu kutoka kwa Rais Gbagbo juu ya kufanya mazungumzo na mpinzani wake Ouattara ili kuweza kumaliza tofauti zao.

Umoja wa Mataifa umearifu kuwa zaidi ya watu 370 wameuawa katika ghasia nchini humo tangu mwishoni mwa mwaka jana, na wengine maelfu kuyakimbia makaazi yao kufuatia mzozo wa kisiasa uliosababishwa na hatua ya Bwana Gbagbo kukataa kukabidhi madaraka kwa mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo uliofanyika Novemba mwaka jana, Alassane Ouattara.

Umoja wa Mataifa tayari umeonya kuwa kwamba nchi hiyo inaweza kutumbukia katika vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vilivyotokea mwaka 2002, ambavyo viligawa nchi hiyo.

Jana Jumatatu waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo waliarifu kudhibiti mji wa tatu ulioko magharibi mwa nchi hiyo baada ya mapigano makali na majeshi yanayomuunga mkono Bwana Gbagbo.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani