1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gesi ya Urusi bado haiwafikii wateja Ulaya.

Sekione Kitojo14 Januari 2009

Urusi ilianza kusafirisha gesi kuelekea katika mataifa ya Ulaya lakini, hadi sasa bado hawafikii walengwa.

https://p.dw.com/p/GY95
Waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin (k) akizungumza na waziri mkuu wa Ukraine Yulia Timoshenko (k) wakati wa mkutano wa during the CSI mjini Chisinau, Moldova hapo Novemba 14 2008.Picha: picture-alliance/ dpa


Furaha juu ya kuanza tena usafirishaji wa gesi kuja katika mataifa ya Ulaya imekuwa kwa muda mfupi tu. Urusi na Ukraine zinaendelea tena kuvutana kuhusiana na upelekaji wa gesi na mataifa mawili ya Ulaya yameanzisha tena juhudi za kidiplomasia ili kumaliza mzozo huu ambao umeziacha nchi hizo bila ya gesi kutoka Urusi kwa muda wa wiki nzima sasa.



Urusi imeanza kusafirisha tena gesi ambayo imelengwa kupelekwa katika mataifa ya Ulaya kupitia Ukraine kuanzia jana , jumanne, lakini umoja wa Ulaya umesema kuwa gesi chache tu ilikuwa inaingia katika mataifa hayo na wakati mwingine haikufika kabisa, kuelekea katika mataifa ambayo yameathirika sana na upungufu wa nishati hiyo. Kiongozi wa kituo cha kusafirisha gesi nchini Urusi cha Sudscha Alexej Fjodorow, aliielezea hali hiyo.

Kwanza kiwango cha gesi kilikuwa kinaonyesha kiasi cha kubiki za ujazo milioni 1.5. Lakini baada ya muda kilipungua, na msukumo ukaanza kupanda. Ilipofika saa sita na dakika 48 kiwango cha gesi kilifika ziro kabisa. Hii ina maana , katika eneo la Ukraine, ambako gesi hiyo inapitia kwa ajili ya wateja wa Ulaya , haikuruhusiwa kupita.

Urusi inaishutumu Ukraine kwa kufunga gesi hiyo inayokwenda katika mataifa ya Ulaya , lakini serikali ya mjini Kiev imesema kuwa hakuna msukumo wa kutosha katika mfumo wa mabomba.

Mzozo huo umeharibu usafirishaji wa gesi katika mataifa karibu 18 wakati wa majira haya ya baridi kali, na kusababisha kufungwa kwa viwanda kadha katika eneo la kusini mashariki ya Ulaya.

Mataifa mawili ya umoja wa Ulaya ambayo yameathirika sana, Bulgaria na Slovakia , yametuma mawaziri wao wakuu nchini Urusi na Ukraine katika juhudi mpya za kuhakikisha kuwa gesi hiyo inapelekwa huko.

Waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico, ambaye alikuwa nchini Ukraine leo kwa mazungumzo na waziri mkuu wa Ukraine Yulia Tymoshenko , amesema kuwa nchi yake ina siku 11 tu za hifadhi ya gesi iliyobaki.

Baada ya siku 12 itabidi kuchukua hatua ambazo hazijawahi kuonekana nchini mwetu, amesema waziri mkuu huyo. Lakini Tymoshenko amesema kuwa nchi yake haiwezi kusaidia.

Fico anatarajiwa kwenda Moscow baadaye leo kukutana na waziri mkuu Vladimir Putin pamoja na waziri mkuu wa Bulgaria Sergei Stanishev pamoja na waziri mkuu wa Moldova Zinaida Greceanii.

Kwa upande wa waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin , anahisi kuwa Ukraine inakwenda kinyume na makubaliano, ambayo yanaelezea kuhusu sheria inayohusu gesi inayopitia nchini humo kuelekea katika mataifa ya Ulaya. Na kwamba Ukraine na Urusi ziangalie udhibiti wa vituo vya usafirishaji wa gesi hiyo. Katika mazungumzo ya simu na rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Mauel Barroso, Putin ameutaka umoja wa Ulaya kuichukulia hatua Ukraine. Viongozi hao pia wamekubaliana kuwa nchi zilizoathirika na mzozo huo ziongeze mbinyo kwa Ukraine.

Putin amesema kuwa amezungumza na mawaziri wakuu wa Slovakia na Bulgaria. Tutakutana mjini Moscow. Viongozi wote hao wanahaja ya kusema kitu, wakija mjini Moscow, kuhusu matatizo yao na msimamo wao.

Makubaliano yaliyofikiwa na umoja wa Ulaya ambayo inapata robo ya mahitaji yao ya gesi kutoka Urusi, yalikuwa na lengo la kurejesha tena upatikanaji wa gesi kuanzia Jumanne jana, ikiwa waangalizi wa kimataifa watawekwa ili kuhakikisha kuwa Ukraine haiibi gesi, kama Urusi inavyodai.


►◄