1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HEILIGENDAMM : Leo ni mkutano wa viongozi wa G8

6 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBuQ

Rais George W. Bush wa Marekani amewasili nchini Ujerumani kwa mkutano wa viongozi wa kundi la mataifa manane G8 katika mji wa mwambao wa Heiligendamm,

Usalama mkali umewekwa katika eneo la mkutano huo ambapo polisi 16,000 wamemwagwa kulinda viongozi wa mataifa yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani. Bush amewasili akitokea katika mji mkuu wa Czech Prague ambapo ametumia hotuba yake kwenye mkutano wa demokrasia na usalama kuitaka Urusi kujiunga na mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami Ulaya ya Mashariki pamoja na kuishutumu nchi hiyo kwa kukwamisha demokrasia.

Bush amesema nchini Urusi mageuzi yalioahidiwa huko nyuma kuwawezesha wananchi yamekwenda kombo na kuathiri vibaya maendeleo ya kidemokrasia.Ameongeza kusema kwamba sehemu ya uhusiano mzuri ni kuweza kujadiliana kwa uwazi kabisa juu ya sitafahamu zao.

Shutuma hizo dhidi ya Urusi yumkini zikazidi kumchafuwa Rais Valdimir Putin wa Urusi ambaye anapinga vikali mipango ya makombora ya kujihami ya Marekani ambayo Marekani inasisitiza kuwa inakusudia kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka vya mashambulizi ya makombora kutoka Iran.

Putin ameonya kwamba mipango hiyo ya Marekani itaifanya Urusi kuelekeza makombora yake yenyewe barani Ulaya na hiyo kuongeza uwezekano wa kuzusha mzozo wa nuklea.

Suala hilo linatishia kugubika mazungumzo juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini barani Afrika ambayo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyapa kipau mbele cha juu katika mkutano huo wa viongozi wa kundi la G8.