1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Historia ya wafanyakazi wa mikataba DDR

2 Novemba 2009

Kuanzia miaka ya mwisho ya miaka ya sitini, Ujerumani ya Mashariki ya zamani ya kisoshalisti DDR ilipohitaji wafanyakazi viwandani mwake, watu hao walitoka nchi za kigeni.

https://p.dw.com/p/KLXu
Wafanyakazi wa Kivietnam nchini DDR kabla ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin 1989.Picha: picture-alliance/ ZB

Mwanzoni, waliletwa kutoka nchi shirika za kikomunisti Poland na Hungary.Lakini kuanzia mwaka 1974 wafanyakazi hao waliojulikana kama wafanyakazi wa mikataba,walitoka nje ya bara Ulaya:yaani kutoka Vietnam, Msumbiji,Angola au Kuba. Je, wafanyakazi hao wanaishi vipi baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mwaka 1989?

Ukuta wa Berlin ulipoanguka mwaka 1989,idadi ya wafanyakazi wa mikataba nchini DDR ilikuwa kama 90,000. Lakini utawala wa kikomunisti uliopotoweka, wafanyakazi hao vile vile walipoteza nafasi zao za ajira, mahala pa kuishi na matumaini ya maisha. Hata hivyo, wengi wao wamebakia huko huko.

Sasa ikiwa ni miongo miwili tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin, maonyesho maalum katika mji mkuu Berlin yanaeleza kile kilichowavutia wakati huo kuja kufanya kazi Ujerumani: vipi walivyokuwa wakiishi katika DDR na hatimae kupewa vibali vya kuishi kihalali katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani baada ya ukuta wa Berlin kuanguka katika mwaka 1989.

Waajiriwa hao wa kigeni walifanya kazi kwa bidii viwandani,machinjoni na katika viwanda vya kemikali. Vile vile walijenga nyumba na barabara - kwa hivyo waliletwa na serikali ya DDR kufanywa kazi nchini humo kwani tangu miaka ya sitini kulikuwepo upungufu mkubwa wa wafanyakzi katika nchi hiyo ya kikomunisti. Sababu ni kuwa baada ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili, wafanyakazi, kwa maelfu, waliipa kisogo nchi hiyo ya mashariki kwa sababu za kisiasa na za kiuchumi na walikwenda kuishi upande wa magharibi.

Sababu nyingine ni kuwa wafanyakazi wengi walihitajiwa kuendesha mashine za kizamani zilizokuwa zikitumiwa viwandani nchini DDR. Lakini ilikuwa nadra kwa serikali kuzungumzia waziwazi kuhusu wafanyakazi hao wa mikataba,kwa vile haikutaka kukiri kuwa kulikuwepo uhaba wa wafanyakazi nchini humo. Hata wananchi wa DDR hawakuarifiwa, wafanyakazi hao wa kigeni walipopelekwa vijijini au katika mitaa ya miji yao. Kwa mfano, Tamara Hentschel anaeishi katika mtaa wa Marzahan mjini Berlin anakumbuka vizuri pale wafanyakazi wa kigeni walipochomoza kwa ghafula katika mtaa wake hapo miaka ya 80.

"Mimi binafsi nilishangazwa sana. Nilikuwa dukani na ninakona watu weusi tele. Nikadhani walikuwa wajumbe wa kigeni. Hakuna mtu aliearifiwa au aliejua sababu za watu hao kuwepo hapo au aliejua kule walikotokea. Hakuna aliejua cho chote."

Maonyesho ya mjini Berlin yametoa sura kamili ya maisha ya wafanyakazi hao wa mikataba katika Ujerumani ya Mashariki ya zamani. Imedhihirika kuwa hali ya maisha yao ilikuwa mbaya kulinganishwa na ile ya Wajerumani. Hentschel anatathmini kuwa idadi ya wafanyakazi wa mikataba nchini DDR ilikuwa kama laki moja na miongoni mwao sitini elfu walitoka Vietnam. Wengi wao baadae walirejea makwao baada ya kulipwa fidia na Ujerumani.Lakini kama Wavietnam 15,000 wameamua kubakia Ujerumani. Kufuatia mageuzi yaliyofanywa katika siasa za haki za wageni, wengi wao katika mwaka 1997 walipewa vibali vya kuishi daima Ujerumani.