1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICRC na Usalama wa Umma Vitani

21 Septemba 2009

Chama cha Msalaba Mwekundu ICRC kilianzishwa zaidi ya miaka 150 iliyopita kwa azma ya kupunguza maafa yanayotokana na vita.

https://p.dw.com/p/JlmW
Die Logos der Internationalen Rotkreuz- und Rothalbmond-Bewegung am Eingang des Internationalen Rotkreuz- und Rothalbmondmuseums in Genf.
Nembo za ICRC.Picha: Julius Kusuma

Harakati za ICRC kote duniani zinahusika na jitahada za kupatanisha mahasimu, kuuguza majeruhi, kutembelea wafungwa wa vitani na wa kisiasa pamoja na kuwalinda raia. Chama cha Msalaba Mkwendu kinahimiza kuheshimiwa kwa haki za kibinadamu- kazi inayozidi kuwa ngumu panapozuka vita vya siku hizi.

Vita kati ya majeshi ya pande mbili katika eneo maalum huku ukiwepo uongozi wa kijeshi unaojulikana waziwazi, ni mambo ya kale. Migogoro ya siku hizi imechukua sura mpya kama Beat Schweizer wa Halmashauri ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu ICRC alivyoshuhudia katika vita mbali mbali kote duniani tangu miaka ishirini iliyopita.Anaeleza hivi:

"Siku hizi vita havina mfumo maalum. Mara nyingi kuna makundi mengi yanayopigana.Mfano mmoja ni Darfur nchini Sudan.Huko kuna zaidi ya makundi kumi na mbili yanayodhibiti silaha.Huwezi kufahamu nani anaeongoza mapigano. Haijulikani ni makundi gani yanayoshirikiana kwani mara hubadili upande wa kuunga mkono."

Hivi sasa, Chama cha Msalaba Mkwendu ICRC, wasaidizi wake katika zaidi ya maeneo 50 ya mivutano kila pembe ya dunia,wanatoa huduma za kiutu. Katika maeneo ya mapigano chama hicho hujaribu kujadiliana na makundi yanayohasimiana na kuomba ruhusa ya kwenda kwa wahanga wa vita. Wakati huo huo, makundi hayo hasimu hushinikizwa kuheshima kanuni za vita kama ilivyokubaliwa karne iliyopita katika sheria za kimataifa kuwatendea binadamu utu. Kanuni hizo zinawataka wanajeshi kuhakikisha usalama wa raia kama iwezekanavyo.

Lakini Beat Schweizer anasema, katika vita vya siku hizi hakuna mipaka kati ya wapiganaji na raia wa kawaida. Katika vita vya desturi, wanajeshi wana sare na hubeba silaha. Raia wana mavazi ya kawaida na wala hawashiriki katika vita hivyo. Lakini katika vita vya siku hizi ni vigumu sana kutofautisha kati ya mpiganaji na raia wa kawaida. Kwa mfano, nchini Afghanistan baadhi ya watu hufanya kazi katika mashamba yao wakati wa mchana lakini usiku unapoingia hujishughulisha na harakati za kijeshi. Watu kama hao, hawana mavazi ya kijeshi na hawabebi silaha wakati wa mchana. Kwa hivyo, si rahisi kulinda usalama wa umma. Ni shida kujua ikiwa anaesaidiwa ni raia asie na hatia au la.

Isitoshe, maeneo ya mapigano yasipokuwa na mipaka dhahiri, raia hawana chaguo jingine isipokuwa kukimbilia kwengineko na mara nyingi familia hutengana . Vita vinapomalizika familia huanza kutafutana. Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wanasema hiyo ni kazi ngumu mno ikilinganishwa na huduma za kuuguza majeruhi, kuwapatia chakula na maji ya kunywa na hata kuwasaidia kujenga nyumba. Kinachowasumbua ni kuona kuwa wahanga wa migogoro hawana matumaini yo yote.

Mwandishi:Claudia Witte/ZR/P.Martin

Mahariri:M.Abdul-Rahman