1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India kuwa kiungo muhimu kati ya mataifa tajiri na yanayoendelea

Sekione Kitojo25 Juni 2007

India , ambayo ilialikwa katika mkutano wa kundi la mataifa tajiri yenye viwabda duniani G8, katika mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Heiligendamm nchini Ujerumani kama moja kati ya nchi tano, uzilizoko nje ya kundi hilo kutoka mataifa ya kusini, hairidhishwi na mataifa hayo ya kaskazini. Inaangalia uwezekano wa pendekezo lililotolewa na nchi nyingine inayoendelea, Brazil , la kuunda kundi jingine ambalo litakuwa linafanya mikutano yake tofauti na kundi la G8.

https://p.dw.com/p/CHCI
Waziri mkuu wa India, Singh, pamoja na washirika wengine wa mkutano wa Heiligendamm
Waziri mkuu wa India, Singh, pamoja na washirika wengine wa mkutano wa HeiligendammPicha: AP

Muungano huu unawezekana ukaitwa kundi la mataifa ya G5, ambayo yatakuwa pamoja na China, Mexico na Afrika kusini , mbali na India na Brazil.

Kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi hizo tano , mawaziri wao wa mambo ya kigeni wanapanga kukutana mjini New York mwezi Septemba , ili kuratibu misimamo wao kuhusiana na masuala ya maslahi yao ya pamoja.

Hata hivyo , wakati ikitafuta muungano huu na mataifa mengine manne makuu, yenye uchumi unaokuwa kwa kasi upande wa kusini, India pia inashiriki katika majadiliano muhimu ya kibiashara katika kundi la mataifa ya kusini na kaskazini la G4, ambalo pia linajumuisha Marekani, umoja wa Ulaya na Brazil.

Mazungumzo ya kundi la G4, yaliyofanyika mapema wiki iliyopita mjini Potsdam nchini Ujerumani, katika mfumo wa ajenda za shirika la biashara la dunia WTO, yamevunjika. Lakini kuna hatua zinazochukuliwa ili kuyafufua upya baadaye mwaka huu. India bado ina imani na mazungumzo hayo.

India itakuwa kiungo muhimu baina ya makundi haya yenye tofauti kubwa, amesema Kamal Mitra Chenoy , profesa wa chuo kikuu cha masomo ya kimataifa cha Jawaharlal Nehru. Haifahamiki ni kiasi gani India itatilia maanani makundi haya pamoja na kuleta maridhiano kutokana na tofauti ya maslahi ya kila kundi.

Matarajio tu ni kwamba India haitajikuta baina ya makundi haya matatu, ameongeza Chenoy.

Mazungumzo ya G4 yamekosolewa mno na chama cha wakulima wa eneo la kusini mwa dunia, pamoja na watu wenye mtazamo wa kimaendeleo , ambao wanaunga mkono kwa dhati serikali kama za Venezuela.

Kuvunjika moyo kwa India na mkutano wa G8 kunatokana na sababu kwamba waziri mkuu Manmohan Singh amehisi , kwa mujibu wa maafisa wa India , kuwa mataifa ya G8 yenye viwanda yanajaribu kuweka ukuta dhidi ya mataifa hayo matano na wanayayumbisha.

Singh amesema kuwa mataifa hayo hayakushiriki kikamilifu katika mijadala na kundi la G8. Kwa hakika taarifa ya pamoja ya kundi la G8 ilitolewa hata kabla ya kukutana nao, na kusema hapo baadaye wanapaswa kupata nafasi ya kujadili masuala yanayowagusa ili mawazo yao yaonekane katika fikra za kundi hilo la G8.

Kwa upande wa pato jumla la kila mwaka , India inatoa kiasi cha asilimia 2 tu ya pato la uchumi wa dunia, na ndogo zaidi kuliko uchumi mdogo kabisa wa nchi za Ulaya magharibi zilizoko katika kundi la mataifa yenye viwanda kama Italia ama Ufaransa, achiliambali Ujerumani ama japan , ambayo ukubwa wake ni mara tatu au nne.

Uchumi wa Marekani ni mkubwa mara 13 kwa India.

India imegawanyika baina ya tamaa ya mambo makubwa na ukweli halisi, kati ya siku zilizopita na usawa wa baina ya mataifa ya kaskazini na kusini na ushirikoano wa mataifa ya kusini, pamoja na uwezekano wa hapo baadaye wa kuwa kama uchumi wenye nguvu.