1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Irak uwanja wa mafunzo kwa magaidi

Mohammed Abdul-Rahman19 Juni 2007

Irak inasemekana sasa imechukua nafasi ya Afghanistan kama ngome ya utoaji mafunzo kwa wapiganaji wanaodai kupigania jihadi, na kusambaza harakati zao katika takriban eneo zima la mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/CHCW
Msikiti wa washia wa Khillani kati kati ya Baghdad,ulioharibiwa katika moja wapo ya mashambulio ya umwagaji damu yanayoendelea nchini Irak
Msikiti wa washia wa Khillani kati kati ya Baghdad,ulioharibiwa katika moja wapo ya mashambulio ya umwagaji damu yanayoendelea nchini IrakPicha: AP

Kizazi kipya cha wanaharakati wa Kiislamu nchini Irak ni chenye ukakamavu zaidi katika uwanja wa mapigano, kuliko maveterani wao wa Kiafghanistan waliopambana na Wasovieti, wakati wa uvamizi wa Urusi nchini Afghanistan . Aidha kusambazwa kwa vita vya jihadi katika nchi ,tulivu zaidi za kiarabu, limegeuka kuwa kusudio lao kubwa.

Kuweko kwa wapiganaji wa kujitolea kutoka Saudi Arabia, Jordan na Yemen katika kambi iliozingirwa ya wapalestina huko Lebanon ya Nahr-al Bared kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na kukamatwa nchini Jordan na Saudi Arabia kwa wanaopigania jihadi kutoka Irak ni ushahidi mmoja wapo.

Marwan Shehaden , mtaalamu wa makundi ya siasa kali katika taasisi ya utafiti kuhusu muelekeo wa hali ilivyo , ilioko mjini Amman-Jordan anasema kwamba upinzani nchini Irak dhidi ya uvamizi hauhitaji waliomo ndani kwani wanaharakati wana wapiganaji wengi , kiasi ya kuwatuma kuna harakati wa kigeni kupigana kwengineko.

Anasema wako tayari kwa hilo, ni watu waliopewa mafunzo kabambe na walio tayari kuendesha vita kokote dhini ya yule wanayemuona adui na sio tu Marekani na Israel, bali hata tawala aza kiarabu zinazopendelea magharibi.

Afisa mmoja wa kibalozi wa magharibi, amesema haoni ni kwa njia gani usambazaji wa itikadi ya vita vya Jihadi unaweza kuzuiwa, akisisitiza kwamba tayari wafuasi wako katika eneo hilo la mashariki ya kati na mambo yamefika mbali, akihofia zaidi msukosuko nchini Jordan.

Mwaka jana mahakama ya kijeshi nchini Jordan niliwahukumu kifo Wasyria watatu na muiraki mmoja kwa kuhusika katika shambulio la kombora dhidi ya manowari ya kimarekani mwezi Agosti 2005, ambapo mwanajeshi mmoja wa Jordan aliuwawa.

Wairaki wengine watatu, Msyria na Mjordan aliyezaliwa Saudi Arabia pia wakahukumiwa vifungo jela kwa kuhusika kwao katika shambulio dhidi ya manowari za kimarekani katika bandari ya Aqaba kwenye bahari nyekundu. Ni mtandao wa Al-Qaeda uliodai kuhusika na hujuma hiyo.

Mwezi Novemba 2005, wairaki waliojitoa mhanga walizilenga shabaha hoteli tatu za fahari mjini Amman na kuwauwa watu 60, wakiwemo wageni. Al Qaeda ikadai tena kuhusika.

Na mwezi Aprili mwaka huu, Jordan ikawahukumu m-Iraki na m-libya kifungo cha maisha, kwa kuhusika katika shambulio la bomu lililoshindwa kwenye uwanja wa ndege wa Amman mwezi Juni mwaka jana 2006, kwa niaba ya Al-Qaeda.

Mtafiti katika kituo cha masuala ya mikakati mjini Amman Mohammed al-Masri anasema “ Barabara moja ya kuelekea Baghdad sasa imegeuka barabara kuu ya pande mbili,” akiongeza wakati kuna wapiganaji wengi wa kujitolea wanaoingia kujiunga na mapigano kuna watu wanaotoka. Irak inasambaza ugaidi. Mtaalamu huyo anaongeza kwamba kupamba moto kwa vita, shehena kubwa ya silaha na miripuko, ukubwa wa miripuko ya mabomu ya kutegwa garini yanayotumiwa na wanaharakati-yote hayo yameigeuza Irak kuwa uwanja mkubwa wa mafunzo.

Katika ripoti ya mwezi Aprili iliotolewa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, mtaalamu wa zamani wa shughuli za upelelezi katika wizara hiyo Dennis Pluchinsky alisema, maveterani wa vita nchini Irak, ndiyo walio hatari zaidi kwa sababu wamepata mafunzo ya hali ya juu kuliko wenzao wa Afghanistan.