1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na mradi wake wa nuklea

Mohammed Abdul-Rahman29 Agosti 2007

Marekani huenda ikashinikiza hatua zaidi za vikwazo, kwani haiamini lengo ni kwa matumizi ya amani tu.

https://p.dw.com/p/CH8p
Kinu cha nuklea cha Busher kusini mwa Iran
Kinu cha nuklea cha Busher kusini mwa IranPicha: dpa

Maafisa wa kibalozi katika makao makuu ya Shirika la kimataifa la nishati ya nuklea IAEA, lenye makao yake makuu mjini Vienna wanasema kwamba ushirikiano wa Iran na wakaguzi wa shirika hilo hauna budi uwe wa kuepusha vikwazo vipya vya umoja wa mataifa mwaka huu. Lakini pamoja na hayo maafisa hao wanasema Iran inapaswa kufungua zaidi milango yake, ili kuondoa kikamilifu kitisho cha hatua za kuiadhibu.

Hivi sasa Iran imeyatatua maswali ya Shirika hilo la nishati ya nuklea la umoja wa mataifa kuhusu majaribio yake kwa matumizi ya plutonium kama kifaa muwafaka cha utengenezaji wa bomu la atomiki. Hayo ni kwa mujibu wa ratiba ya kikazi baina ya shirika hilo na Iran iliotolewa na Iran kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Vienna-Austria mapema juma hili.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, inaelezwa kwamba Iran pia iko tayari kutatua maswala yanayozusha wasi wasi kuhusiana na nyaraka zinazodaiwa zinaashiria katika kuweko kwa mradi wa siri wa kijeshi kwa ajili ya kutengeneza bomu la nuklea.

Maswala mengine ni pamoja na shughuli za irak zinazohusiana na urutubishaji wa madini ya uranium na ujenzi wake wa kinu cha maji mazito kwa ajili ya utengenezaji plutonium. Madini yote hayo mawili yanaweza kutumiwa kwa ajili ya kinu cha nuklea na pia katika sehemu ya mripuko wenyewe ndani ya bomu la nuklea.

Afisa mmoja wa kibalozi alisema lengo ni kwa Iran kutoa majibu ya maswali yote yaliosalia kutokana na uchunguzi wa IAEA hadi ifikapo mwezi Desemba, ambapo baada ya miaka minne bado halijaridhika kwamba mradi wa Iran ni kwa ajili ya amani.

Madai ya Marekani ni kwamba Iran inautumia mradi huo kama kinga tu lakini lengo ni kutengeneza silaha za nuklea na inasema Iran inacheza tu na shirika hilo la kimataifa la nishati ya nuklea, ili kuepuka vikwazo zaidi vya umoja wa mataifa.

Marekani inashikilia kwamba Iran haiwezi kuruhusiwe iepukane na sehemu mbili vza vikwazo vya wakati huu vyenye lengo la kuilazimisha isitishe urutubishaji wa uranium.

Mjini Teheran Rais Mahmoud Ahmedinejad alisema mnamo siku ya Jumanne kwamba Iran inalichukulia swala hilo kuwa sasa limetatuliwa, akiwaambia waandishi habari “ kwa mtazamo wetu sisi, ukurasa umeshafungwa kuhusu kisa cha Iran kuhusu nuklea .” na kuongeza “Iran ni taifa la kinuklea.”

Lakini Marekani na pia wanachama wenzake wa kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa-Uingereza na Ufaransa- zinashinikiza duru ya tatu ya vikwazo, ingawa Urusi na China zinataka kwanza kuona matokeo ya ushirikiano wa shirika la kimataifa la nishati ya nuklea na Iran unavyoendelea.

Tayari mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo na shirika hilo Ali Larijani ameonya kwamba ikiwa Marekani itawashinikiza washirika wake kuchukua hatua zaidi na baraza la usalama kufanya hivyo basi swala hilo kwa upande wa Iran litakua limemalizika na ushirikiano na shirika hilo la kimataifa la nishati ya nuklea utakua umeingia dosari.

Mtaalamu wa maswala yanayaohusiana kuzuiwa utapakazaji silaha za maangamizi Mark Fitzpatrick alisema mjini London kwamba anafikiri kuwa Iran imecheza vyema karata zake ambazo zinaweza mno kuchelewesaha hatua nyengine zozote za ziada dhidi yake katika baraza la usalama hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Bw Firtzpatrick na maafisa kadhaa wakibalozi pia wameelezea wasi wasi wao juu ya ratiba iliowasilishwa kwa iran ikitakiwa kujibu maswali yote yaliosalia na kutokuwepo tena kwa maswala ya ziada. Anasisitiza kuwa cha kuzingatiwa ni kwamba kila swali lililojibiwa limezusha maswali ya ziada na mengine yaliojibiwa majibu hayajakamilika.