1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yajitolea kuisaidia Misri kutatua tatizo la Gaza

28 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CyX4

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Misri, Ahmed Aboul Gheit, amesema Iran imejitolea kuisadia Misri kutatua tatizo linalozidi katika mpaka wake na eneo la Ukanda wa Gaza.

Ahadi hiyo nadra ya Iran imetolewa wakati wa ziara ya mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran, Ali Asghar Mohammadi, mjini Cairo.

Kiongozi huyo wa Iran ni mkurugenzi katika wizara ya mashauri ya kigeni ya Iran anayehusika na maswala ya nchi za kiarabu, mashariki ya kati na Afrika Kaskazini.

Misri na Iran hazijakuwa na uhusiano rasmi kwa karibu miongo mitatu lakini mawaziri wa nchi hizo mbili wamekuwa wakikutana mara kwa mara katika miezi miwili iliyopita.

Maelfu ya wapalestina wamerejea katika makazi yao huko Gaza baada ya Misri kukatiza usafirishaji wa bidhaa na kulidhibiti eneo la mpakani.

Polisi wa kupambana na fujo wa Misri pamoja na wanajeshi walishika doria katika kivuko cha mpakani cha Rafah huku usalama ukiimarishwa huko Sinai na kuzuia malori yaliyokuwa yakiwapelekea bidhaa muhimu wapalestina waliokuwa wakiendelea kuvuka mpaka kati ya Misiri na Gaza kwa siku ya tano.

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert na rais wa mamlaka ya ndani ya Plaestina, Mahmoud Abbas, wameahidi kuzuia kutokea kwa janga la kibindamu katika Ukanda wa Gaza, baada ya kukutana huko mjini Jerusalem, Israel.