1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaridhia kushiriki mazungumzo juu ya silaha za nyuklia

MjahidA27 Septemba 2013

Maafisa wa ngazi ya juu wa Iran na wale wa shirika la UN la kudhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki-IAEA, wameanza majadiliano mjini Vienna juu ya uchunguzi wa mpango wa silaha za nyuklia za Iran.

https://p.dw.com/p/19pN0
Wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
Wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa MataifaPicha: Stan Honda/AFP/Getty Images

Haya ni mazungumzo ya kwanza kufanywa tangu kuchaguliwa kwa Hassan Rowhani kama rais mpya wa Iran.

Mkutano huu wa leo unafanyika siku moja baada ya mawaziri wa nchi za nje wa nchi tano wanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kukutana na waziri mwenzao wa Iran na kukubaliana kuyafufua tena mazungumzo juu ya silaha za nyuklia za Iran.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika katikati ya mwezi ujao mjini Geneva.

I"Tunakaribisha maendeleo ya hivi karibuni na tamko kutoka Iran kwamba wanaridhia kuwa katika mazungumzo ya nyuklia," Alisema mkuu wa uchunguzi katika shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki-IAEA Herman Nackaerts.

Mkuu wa uchunguzi katika shirika la IAEA Herman Nackaerts
Mkuu wa uchunguzi katika shirika la IAEA Herman NackaertsPicha: AP

ran kwa upande wake kupitia waziri wake mambo ya nje Mohammad Javad Zarif, imesema ingelipenda kuanza mazungumzo hayo haraka iwezekanavyo ili kuwezesha vikwazo kuondolewa dhidi yao, vikwazo ambavyo vimechangia katika kuanguka kwa uchumi wa Iran.

Tunaamini vikwazo havina manufaa yoyote vinaleta athari kubwa na haviendi sambamba na sheria za kimataifa hakika tukisonga mbele lazima kuondolewe vikwazo na tunaamini tutaelekea katika njia hiyo katika muda mfupi ujao," Alisema waziri Javad Zarif .

Iran hata hivyo imekana kuwa ina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia lakini taasisi ya nyuklia ilioko Viena imesema ina ushahidi unaoonesha nchi hiyo inatengeneza silaha hizo.

Urusi na Marekani zakubaliana juu ya Syria

Wakati huo huo katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika mjini NewYork, Marekani na Urusi kwa pamoja zimekubaliana juu ya azimio la baraza la usalama la umoja wa Mataifa la kuitaka Syria kutoa silaha zake zote za sumu.

Lakini katika azimio hilo hakuna tishio lolote la nchi hiyo kuingiliwa kijeshi iwapo haitatoa silaha hizo. Samantha Power balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema....

"Hii ni muhimu sana, hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita nchini Syria miaka miwili na nusu iliopita ambapo baraza la usalama la umoja wa mataifa limeweka sheria juu ya Syria zinazolazimisha nchi zote kufuata," Alisema Power.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry wa Marekani na Sergei Lavrov wa Urusi.
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje John Kerry wa Marekani na Sergei Lavrov wa Urusi.Picha: Reuters

Marekani inaendelea kudai kuwa rais wa Syria, Bashar al Assad, ametumia silaha za sumu dhidi ya raia wake katika shambulizi lililowauwa zaidi ya raia 1,400. Hata hivyo Syria pamoja na Urusi wanasema waasi ndio waliohusika na shambulizi hilo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mwandishi: Amina Abubakar dpa/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo