1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaupokea mkono wa Obama kwa masharti.

28 Januari 2009

Iran haitaki badiliko la mbinu tu .

https://p.dw.com/p/Gi2h
Mahmoud AhmadinejadPicha: AP

Iran imearifu kwamba itaupokea mkono ilionyoshewa na Rais Barack Obama wa badiliko la siasa kwa sharti kuwa, utajumuisha pia Marekani kuondoa majeshi yake kutoka nchi za ngambo.Isitoshe, Marekani itake radhi kwa "uhalifu iliofanyia Iran siku za nyuma .

Katika mahojiano yake ya kwanza kabisa na chombo cha habari tangu kutawazwa Rais,Barack Hussein Obama na kituo cha TV cha "Al Arabiya",aliitaka Iran iache kuviringa ngumi.

Serikali mpya ya Marekani inapaswa kufanya mabadiliko makubwa katika sera zake na sio tu katika mbinu zake-alisema Rais Ahmadinejad leo baada ya Rais Barack Obama kuinyoshea Iran mkono wa suluhu. Akaongeza,

"Wanaposema wanataka kubadili,basi mabadilłiko yaweza kuwa ya aina mbili......Njia ya pili ni kubadili mbinu."Alisema Ahmadinejad akihutubia mkutano wa hadhara huko magharibi ya Iran.

"ni wazi kabisa ikiwa tafsiri ya badiliko ni njia hii ya pili,hii haitakawia kubainika."-alisema.

Msimamo wa serikali mpya ya Marekani ni tofauti na ule wa serikali ilipita ya George Bush aliechukua hatua za kuitenga Iran na wanadiplomasia wa kambi ya magharibi wamesema badiliko la sera huko Washington laweza likatoa fursa inayoibuka mara moja tu katika kizazi kwa mahasimu hawa wawili kukomesha miongo 3 ya uchokozi.

Wanadiplomasia wamesema lakini ,kwamba wakati baadhi ya sauti za wastani huko Teheran zinalilia usuhuba bora na nchi za magharibi,zile za wakakamavu zenye kudhibiti hatamu za uongozi zaweza zikazima juhudi hizi kwa kuchelea kuwa Marekani ingali ina nia ya kutokomeza utawala wa sasa wa Iran.

Rais Ahmadinejad amesema kuwa,badiliko la mbinu tu za kisiasa litabainika haraka.Wale wanaodai wanataka mabadiliko , wanapaswa kwanza kuomba radhi kwa taifa la Iran na kufuta madhambi waliolifanyia taifa la Iran-aliongeza rais wa Iran.

Uamuzi wowote wa kuwa na mazungumzo ya pande mbili-Iran na Marekani, yatahitaji kwanza idhini ya Imam Mkuu,Ayatollah Ali Khamednei,mwenye mamlaka ya mwisho nchini Iran.

Nae alisema oktoba mwaka jana kwamba chuki juu ya Marekani ni kubwa miongoni mwa wairani na akawaonya mwezi huu viongozi wa Irak kwamba serikali za Marekani haziaminiki.

Utawala mpya wa Washington, umesema kuwa, utaachana na sera za ule ulioutangulia kwa kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Teheran.Lakini, wakati huo huo, ulionya kuwa Iran itarajie kutiwa shindo kubwa endapo haitalitekeleza Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloitakya kuachana kabisa na mradi wake wa kinuklia unaozusha mvutano.

Marekani na washirika wake wa Kambi ya Magharibi, wanaituhumu Iran kuwa na azma ya kuunda bomu la atomiki ;wakati Iran inakanusha na inabisha kuacha na mradi wake ikiitetea haki yake ya kufanya hivyo kama nchi huru.

Rais Ahmadinejad wa Iran ameorodhesha madhambi kadhaa Marekani ilioifanyia Iran mfano kuzuwia mradi wake wa amani wa nishati ya kinuklia, kuzuwia maendeleo ya Iran tangu mappinduzi ya jamhuri hiyo ya kiislamu 1979-na vitimbi vyengine iliofanyiwa na serikali tofauti za Marekani mnamo miaka 60 iliopita.