1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ireland yasisitiza kuwa haihitaji msaada wa kifedha.

17 Novemba 2010

Wachunguzi wanadai huenda Ireland itahitaji Euro bilioni 70 ili kuifufua sekta ya benki.

https://p.dw.com/p/QB4P
Ireland ina nakisi kubwa ya bajeti mwaka huu.

Ulaya na shirika la fedha duniani, IMF, zimetangaza nia ya kuzindua mikakati ya dharura ya kifedha kuikwamua sekta ya mabenki ya Ireland ambayo yanakumbwa na mzozo. Hata hivyo, taifa hilo mwanachama wa Umoja wa Ulaya halijakubali wazi wazi kwamba linakumbwa na kitisho cha kufilisika.

Kuwasili kwa wataalam nchini Ireland kutoka tume ya Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Umoja huo na wale wa shirika la fedha duniani, IMF, kumekuwa ni pigo kwa taifa hilo ambalo linadai linaweza kukidhi mahitaji yake na hadi kufikia sasa halijakubali msaada wa fedha.

Hali hiyo imezusha wasiwasi kati ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa sababu mzozo wa kifedha katika sekta ya benki nchini Ireland umesababisha nakisi ya bajeti ya nchi hiyo kuwa zaidi ya asilimia 30 ya pato lake la ndani mwaka huu.

Hayo yanajiri wakati ambapo mawaziri wa fedha wa Umoja huo walikutana mjini Brussels kujadili hatima ya Ireland. Waziri wa fedha wa Ireland, Brian Lenihan aliwasili akiwa amechelewa kwa masaa mawili katika mkutano huo ambapo waziri mkuu wake alikuwa akisisitiza kwamba hawajaomba msaada wa dharura. Muda mfupi baadaye, waziri huyo wa fedha, Bw Lenihan alikiri kwamba uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya Ireland uko karibu kutolewa. Alisema maendeleo hayajakuwa mazuri kwa Ireland katika wiki za hivi karibuni, na alidokeza kwamba Ireland inaweza kukidhi matumizi ya fedha hadi mwaka ujao na kwamba kuna changamoto katika soko.

EU Logo mit Karte und Flagge 2010 Grafik: DW-Grafik, Olof Pock Datum 06.01.2010
Umoja wa Ulaya una wasiwasi na Ireland. Dhamana ya sarafu ya Euro imeshuka japo kwa senti chache.

Waziri mkuu wa Luxembourg, Jean-Claude Junker, amesema ikiwa itawalazimu, watachukua hatua madhubuti kuhakikisha uimara wa kanda inayotumia sarafu ya Euro. Junker, ambaye ni mwenyekiti wa mawaziri wa fedha katika Umoja huo, amesema katika siku chache zijazo lazima Ireland iamue hatima ya msaada wa kifedha utakaokuwa na masharti.

Rais wa Umoja huo, Herman van Rompuy, akigusia mjadala huo kwa ujumla na huku Ureno pia ikikumbwa na kitisho cha kufilisika, alisema mwaka wa kwanza tangu kusainiwa, mkataba wa Lisbon umekumbwa na mzozo katika kanda inayotumia sarafu ya Euro. Lakini alisisitza kwamba hiyo haimaanishi kuwa mwaka wa 2010 ni mwaka wa mzozo na wamedhihirisha wanaweza kukabiliana na mzozo na wataibuka kwa ushindi.

Jumuiya ya Ulaya inajizatiti kudhihirisha kwamba ilipata funzo kutokana na msaada wa Euro bilioni 110 uliotumiwa kuikwamua Ugiriki na wachunguzi wanadai kwamba huenda Ireland itahitaji takriban Euro bilioni 70.

Huku hayo yakijiri, waziri wa fedha wa Uingereza, George Osborne, amesema nchi yake iko tayari kushiriki kutoa msaada kwa Ireland kwa sababu ni taifa jirani.

Taswira hiyo imesababisha dhamana ya sarafu ya Euro kushuka na ilibadilishana kwa Dola 1.35 ya Kimarekani, hasa baada ya mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kushindwa kuafikiana baada ya mkutano wao uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji.

Mwandishi: Peter Moss /AFP/AP

Mhariri: Othman Miraji.