1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiMashariki ya Kati

Israel: ICJ itupilie mbali kesi ya mauaji ya kimbari

Angela Mdungu
12 Januari 2024

Israel imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya ICJ kuitupilia mbali kesi inayoituhumu nchi hiyo kufanya "mauaji ya halaiki" huko Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4bB2y
Uholanzi | Mahakama ya Haki ya Kimataifa ICJ
Mshauri wa masuala ya Kisheria wa Israel Tal Becker akiwa katika mahakama ya ICJPicha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Katika siku ya pili ya kuisikiliza kesi iliyowasilishwa na Afrika ya Kusini, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Israel Gilad Noam amesema kuwa kesi hiyo haina hoja za msingi.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Israel Gilad Noam, amedai kuwa Israel imetimiza majukumu yake yote ya kisheria. Wakati Israel ikijitetea Ijumaa dhidi ya tuhuma za Afrika ya kusini zinazodai kuwa inafanya vitendo sawa na mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza, mwakilishi wa Israel katika kesi hiyo Galit Raguan ametetea juhudi za nchi hiyo za kupunguza madhara kwa raia na kutolea ufafanuzi kuhusu hali ya kiutu katika Ukanda huo.

Soma zaidi: Israel yajibu tuhuma za Afrika ya Kusini mbele ya ICJ

Raguan amekanusha tuhuma za kufanya mauaji ya halaiki kwa makusudi  na kudai kuwa Israel ilichelewesha mashambulizi ya kijeshi ya ardhini kwa wiki kadhaa ili kuwaruhusu raia wa Gaza kutafuta maeneo salama. Mwakilishi huyo wa Israel amezungumzia pia uwekezaji katika rasilimali uliofanywa na Israel ili kuwapa raia maelezo kuhusu mahala pa kwenda na namna ya kuondoka kwenye sehemu zenye mapigano.

Uholanzi | Mahakama ya Haki ya Kimataifa ya ICJ
Mahakama ya ICJ ikisikiliza kesi iliyowasilishwa na Afrika ya Kusini dhidi ya IsraelPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Alihitimisha kwa kusema kuwa, juhudi za Israel za kupunguza madhara ya vita kwa raia ni kinyume cha kufanya uharibifu kwa kukusudia na hivyo kuzifanya tuhuma za mauaji ya halaiki kwa kusudia kukosa uzito.

WHO: Hospitali ya Al-Shifa imerejesha sehemu ya huduma zake

Kwingineko, Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa Hospitali kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza ya Al-Shifa, iliyoaharibiwa na vita vya Israel dhidi ya Hamas, imeanza kurejesha sehemu ya huduma zake.

Ukanda wa Gaza | Timu ya WHO kwenye hospitali ya Al Shifa
Timu ya WHO ilipoitembelea hospitali ya Al Shifa mwezi Novemba, 2023 Picha: WHO/REUTERS

Soma zaidi: Afrika Kusini yaishutumu Israel kwa mauaji ya kimbari

Naye mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO  Tedros Gebreyesus kupitia mtandao wa X amesema kuwa kwa sasa hospitali hiyo ya Al Shifa iliyositisha huduma zake kwa kiasi kikubwa mwezi Novemba baada ya operesheni za kijeshi za Israel sasa ina wahudumu wa afya 60. Amesema hospitali hiyo ina wodi ya upasuaji na matibabu yenye vitanda 40, kitengo cha dharura na vyumba vinne vya upasuaji na khuduma za kina mama.