1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yakabiliwa na ukosoaji kufuatia vita huko Gaza

15 Desemba 2023

Wakati viongozi mbalimbali duniani wakiendelea na juhudi za kuhimiza usitishwaji mapigano, Israel imeibua ukosoaji wa nadra kutoka Marekani na ghadhabu ya kimataifa kufuatia vita huko Gaza.

https://p.dw.com/p/4aBKB
Gazastreifen, Rafah | Zerstörungen nach einem Israelischen AngriffIsrael Palestinians
WaPalestina wakishuhudia uharibifu mkubwa huko Rafah baada ya shambulizi la Israel katika tukio la Novemba 14, 2023Picha: Hatem Ali/AP/picture alliance

Gaza imeendelea kushuhudia mashambulizi ya vikosi vya Israel, ambapo usiku wa jana, kampuni kuu za mawasiliano katika Ukanda huo ambazo ni Paltel na Jawwal, zilisema kuwa huduma zote za simu na intaneti zilikatika. Mji wa Rafah ulishambuliwa pia usiku wa kuamkia leo. Bakr Abu Hajjaj, ni mkazi wa kitongoji hicho:

" Tulikuwa tumelala kwenye nyumba yetu na ghafla kukatokea shambulio lililosikika kama bomu. Kuna watu waliojeruhiwa, kila kitu kimeharibiwa. Ni siku 70 sasa tumekuwa tukishuhudia vita hivi na uharibifu."

Waziri Mkuu wa Israel  Benjamin Netanyahu  amemueleza mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Jake Sullivan kuwa Israel itaendeleza vita vyake dhidi ya Hamas hadi wapate ushindi kamili. Lakini Sullivan amejibu kauli hiyo leo kuwa Marekani inataka kuona matokeo kuhusu nia ya Israel ya kuepusha madhara kwa raia.

Israel | Treffen Jake Sullivan mit Yoav Gallant
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant (kulia) akisalimiana na mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Jake Sullivan mjini Tel-Aviv: 14.12.2023Picha: GPO/Anadolu/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali mjini Tel-Aviv, Netanyahu na Sullivan walizungumzia pia kuhusu vitisho vya kikanda ikiwa ni pamoja na kundi la Hezbollah nchini Lebanon na waasi wa Houthis kutoka Yemen. Pia walijadili juhudi za kuwaokoa mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas pamoja na suala la misaada ya kibinadamu kwa raia huko Gaza.

Soma pia: Matajiri Uganda wachangia dola milioni 50 kwa Israel, Gaza

Sullivan anatarajiwa pia leo hii kufanya mazungumzo na rais wa mamlaka ya Palestina  Mahmoud Abbas ili kujadili mipango ya baada ya vita katika Ukanda wa Gaza, ambayo kulingana na taarifa iliyotolewa na Sullivan inaweza kujumuisha kuanzishwa tena kwa vikosi vya usalama vya Palestina ambavyo vilisambaratishwa na kundi la Hamas mwaka 2007.

Miito ya suluhisho ya serikali mbili na usitishwaji vita

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Palestina amesema katika mahojiano kuwa utawala wa Biden unatakiwa kuchukua hatua muhimu na kuishinikiza Israel kuelekea jambo ambalo amesema limekuwa gumu kupatiwa suluhisho la serikali mbili.Lakini Israel imesema huu si wakati wa kujadili suluhisho kama hilo.

Palästinensische Autonomiegebiete | Besuch Antony Blinken in Ramallah
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken (kushoto) akisalimiana na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas mjini Ramallah: 30.11.2023Picha: Saul Loeb/AP Photo/picture alliance

Israel imesema wanajeshi wake 116 wamekufa tangu kuanza kwa operesheni yao ya ardhini huko Gaza baada ya Hamas kuvamia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 na kuua watu wapatao 1,200 na kuwachukua mateka wengine takriban 240. Waziri wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, ameeleza kuwa itachukua miezi kadhaa kuwashinda kabisa kundi la Hamas.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemwambia Rais Joe Biden kwamba Marekani ina "jukumu la kihistoria" la kufikia haraka iwezekanavyo makubaliano ya usitishaji kamili wa vita,  na kwamba hilo linaweza kufikiwa haraka ikiwa Marekani itasitisha uungaji wake mkono kwa Israel. Erdogan ameonya kwamba "mashambulizi ya muda mrefu ya Israel huko Gaza yanaweza kuwa na matokeo mabaya kote duniani."

(Vyanzo: Mashirika)