1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utanuzi wa vita vya Israel Gaza Kusini wazidisha wasiwasi

Iddi Ssessanga
4 Desemba 2023

Israel imetanua vita vyake dhidi ya Hamas katika maeneo ya kusini mwa Gaza, licha ya wasiwasi wa kimataifa juu ya vifo vya raia vinavyoongezeka na hofu kwamba mzozo huo utasambaa kwingineko katika Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4Zlne
Vita vya Israel-Hamas | Mashabulizi ya ndege Khan Younis.
Wapalestina wakikimbia kufuatia mashambulizi ya ndege za Israel katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Gaza.Picha: Saleh Salem/REUTERS

Mashuhuda wamesema Israel imevielekeza vikosi vyake vya ardhini kusini mwa Gaza katika vita vyake dhidi ya Hamas, licha ya wasiwasi wa kimataifa juu ya vifo vya raia vinavyoongezeka na hofu kwamba mzozo huo utasambaa kwingineko katika Mashariki ya Kati.

Vita hivyo tayari vimeua maelfu ya Wapalestina na kuwakosesha makazi zaidi ya theluthi mbili ya wakazi milioni 2.3 wa Gaza, ambao wanaishiwa maeneo ya kukimbilia.

Vifaru vya jeshi, magari ya kivita na tingatiga vimeshuhudiwa vikiingia kusini mwa Gaza, vikiwa karibu na mji wa pili kwa ukubwa wa eneo hilo, wa Khan Younis leo Jumatatu, wakati Israel ikitanua operesheni zake.

Shuhuda moja kwa jina la Gazan Amin Abu Hawli, amesema vifaru hivyo vya Israel vilikuwa umbali wa karibu kilomita mbili ndani ya Gaza, katika kijiji cha Al-Qarara karibu na Khan Younis.

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas: IDF yatanua mashambulizi ya ardhini Gaza

Jeshi la Israel limesema lilikuwa linachukuwa hatua kali dhidi ya Hamas na makundi mengi ya kigaidi katika mji huo wa kusini.

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, Mirjana Spoljaric, amesema kupitia mtandao wa X kwamba amewasili Gaza, na kuonya kwamba mateso wanayopita wakazi wa eneo hilo hayavumiliki.

Ukanda wa Gaza| Mashambulizi dhidi ya mji wa Khan Younis.
Moshi ukitoka katika jengo lililoharibiwa mjini Khan Younis, katikati mwa mapambano yanayoendelea kusini mwa Gaza, Desemba 4, 2023.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Spoljaric amerudia wito wa kulindwa kwa raia kwa kufuata sheria za kivita, na kuruhusu msaada kuingia bila vizuwizi vyovyote. Ameongeza kuwa mateka wanapaswa kuachiwa na ICRC kuruhusiwa kuwatembelea kwa usalama.

Msmaji wa jeshi Jonathan Conricus, amesema Israel haijaribu "kumhamisha mtu yeyote,"  na kuongeza kuwa wameainisha maeneo ya kibinadamu ndani ya Ukanda wa Gaza, akimaanisha eneo dogo sana la pwani liitwalo Al-Mawasi.

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, alielezea wasiwasi kwamba mamia ya maelfu ya Wagaza walikuwa wanarundikwa katika maeneo madogo sana ya Kusini.

Wapalestina wengi wanahofia kurudiwa kwa  kilichotokea miaka 75 iliyopita, kufurushwa kwa  wenzao 760,000, kulikotokea wakati wa vita vilivyopelekea kuundwa kwa taifa la Israel  katika kile kinachojulikana kama Nakba.

Erdogan asema Netanyahu atashtakiwa kwa uhalifu wa kivita

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Waziri Mkuu Wa Israel  atashtakiwa kwa madai ya uhalifu wa kivita kama ilivyokuwa kwa rais wa zamani wa Serbia Slobodan Milosevic. 

Soma pia: Waislamu wajihisi hawako salama UIaya

Akizungumza kwenye mkutano wa kilele wa mawaziri wa shirika la ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu mjini Istanbul, Erdogan amemuita Netanyahu kuwa "mchinjaji wa Gaza", na kuongeza kuwa atashtakiwa kama alivyoshtakiwa Molosevic mjini The Hague, kwa kuhusishwa na uhalifu wa kivita uliotendekea katika vita vya Yugoslavia.

Erdogan pia amerudia ukosoaji wake wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, na kuyatuhumu mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuzuwia juhudi za kukomesha machafuko.

"Kwa upande mmoja, kuna mataifa 121 yanayosema simamisheni vita na hakuna umuagaji tena wa damu, na kwa upande mwingine, kuna mataifa matatu hadi matano yanaoidhinisha mashambulizi ya Israel," alisema Erdogan.

Erdogan aakihutubia mkutano wa OIC
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atashtakiwa kwa uhalifu wa kivita.Picha: Murat Kula/Anadolu/picture alliance

"Kuna mfumo wa kimataifa ambao unachukuwa hatua tu pale mataifa haya matano yanapotoa idhini. Haiwezekani kwa muundo kama huo kueleta amani, kusimamisha mzozo, au kutoa matumaini kwa binadamu," aliongeza.

Vita hivyo tayari vimeua maelfu ya Wapalestina na kuwakosesha makazi zaidi ya theluthi mbili ya wakazi milioni 2.3 wa Gaza, ambao wanazidi kuishiwa maeneo salama ya kwenda.

Soma pia:Israel yaamuru watu kuyahama maeneo zaidi Ukanda wa Gaza 

Wizara ya afya ya Gaza iliyoko chini ya Hamas, inasema idadi ya vifo tangu Oktoba 7 imefikia 15, 899, ambapo asilimia 70 kati yao ni wanawake na watoto, na zaidi ya 41,000 wamejeruhiwa.

Israel inasema inalenga watendaji wa Hamas na kulaumu maafa ya kiraia kwa wapiganaji hao inaowatuhumu kuendesha shughuli zao katika maeneo ya makaazi. Inadai kuwa imeua maelfu ya wapiganaji, bila hata hivyo kutoa ushahidi, na imesema wanajeshi wake wasiopungua 81 wameuawa katika vita hivyo.

Matumaini ya mapatano mengine ya kusitisha vita kwa muda yalififia baada ya Israel kuwarejesha nyumbani wapatanishi wake mwishoni mwa wiki.

Israel na Hamas wameanza tena mapigano

Hamas ilisema mazungumzo juu ya kuachiliwa mateka wengine yanapaswa kuambatana na usitishaji mapigano wa kudumu.

Marekani, pamoja na Qatar na Misri, zilizoratibu usitishaji wa kwanza wa mapigano, zimesema zinafanyia kazi mapatano ya muda mrefu ya kusitisha vita.

Chanzo: Mashirika