1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

140911 Italien China

14 Septemba 2011

Italia, ambalo ni taifa la tatu kwa uchumi mkubwa kwenye eneo la Sarafu ya Euro, inaripotiwa sasa kuomba msaada wa China ili kujikwamua na uwezekano wa kuanguka kiuchumi na tayari mazungumzo ya awali yameshafanyika.

https://p.dw.com/p/12YuP
Sarafu za China na za Ulaya, mshikamano wa wasiwasi?
Sarafu za China na za Ulaya, mshikamano wa wasiwasi?Picha: Gina Sanders/Fotolia.com

Licha ya kuanza kutoka kauli za kukanusha ripoti ya gazeti la Financial Times la hapo jana, kwamba Italia sasa inaiomba China izinunue dhamana zake, jambo lisilo siri ni kuwa kwa siku za hivi karibuni Italia imekuwa kifuu-tomo.

Mabilioni ya euro yameingizwa katika mfuko wa mikopo wa Italia kutokea Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya, na bado hakuna dalili kuwa nusura ya uchumi wa nchi hiyo ipo karibu.

Kilichopo ni kinyume chake: kiwango cha deni la Italia hakisemeki, na kwa hakika hasa kimefikia rikodi ambayo haijawahi kufikiwa hata kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katikati ya mgogoro huu wa madeni, Italia imejikuta ikielekeza mkono wake China kuomba msaada. Katika wiki zilizopita kumekuwa na mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha wa Italia, Giulio Tremonti na Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa China, Lou Jiwei.

Mtaalamu wa masuala ya China katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mailand, Giuliano Noci, anasema kuwa undani wa mazungumzo ya Tremonti na Jiwei unaweza kuhesabika kwa vidole vitano tu vya mkono.

"Kwa sasa China ina akiba ya kutosha: dola bilioni 3,200, ni kiwango kikubwa sana, ni mara mbili zaidi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi hiyo. Kwa hivyo, ni jambo la kawaida kwamba China inaelekeza maslahi yake Ulaya na Italia, na hilo kawaida linafanyika kwa kufikiria faida."

China inakusudia kufanya biashara ya madeni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini (kushoto), na mwenzake wa Ugiriki, Stavros Lambrinidis, wote nchi zao zimekabiliwa na mzozo wa madeni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Frattini (kushoto), na mwenzake wa Ugiriki, Stavros Lambrinidis, wote nchi zao zimekabiliwa na mzozo wa madeni.Picha: dapd

Hiyo ni kusema kuwa sio kwamba China itakuwa kama msamaria mwema aliyeshuka kuja kulisaidia deni la Italia tu, bali ni muwekezaji anayekuja kutengeneza faida kubwa kupitia deni hilo.

Matarajio hayo hayo tayari yapo kwa mataifa mengine ya eneo la Sarafu ya Euro yaliyokumbwa na kupaa kwa deni lake, yakiwemo Ugiriki na Ureno.

Wataalamu wanasema kwamba China inataka kuwekeza katika sekta muhimu nchini Italia za teknolojia na nishati. Johari hizi za Italia, kama zinavyoitwa, bado kwa kiasi kikubwa zimo kwenye mikono ya serikali. Uingiliaji kati wa China utaingiza fedha za kutosha katika makasha ya sekta hizo.

"Kwa hakika Wachina wana maslahi makubwa kwenye johari zetu na kwa upande mwengine wangelitaka uungwaji mkono katika kiwango cha siasa za kimataifa. Katika mazingira kama haya, Wachina wanaweza kuchukuwa jukumu kwenye deni letu la taifa na matokeo yake wangelitaka kuona kuwa China na Italia zinashirikiana na zinasaidiana katika jukwaa la kimataifa." Anasema Noci.

Ni biashara yenye maslahi kwa pande zote mbili. Si kipindi kirefu kilichopita, ambapo Waziri wa Fedha wa Italia Tremonti na Waziri wake Mkuu Silvio Berlusconi walikuwa wakipingana na kuongezeka kwa bidhaa za China katika soko lao la ndani.

Lakini sasa, Tremonti ameiacha ngome ya Ulaya na kuigeukia China kuomba uwekezaji. Na Berlusconi anakwenda makao makuu ya Umoja wa Ulaya, mjini Brussels, kwenda kuimarisha uhusiano na washirika wa Ulaya.

Berlusconi anafanya kile anachoamini kitamuwezesha kuhimili mikiki ya kisiasa: ndani ya nchi yake anapambana na upinzani mkali na ameamua kusimama imara na mkaidi, akisema kwamba Italia haina tatizo la madeni.

"Sekta binafsi, makampuni, familia, mabenki, wote wana utulivu wa kifedha. Familia za Waitalia zimeweka akiba. Mtu anapolinganisha deni la taifa na uwezo wa makampuni na familia za Waitalia, anakuta kuwa tuko nyuma ya Ujerumani tu, miongoni mwa mataifa yote ya Umoja wa Ulaya". Ndivyo anavyosema Berlusconi.

Lakini ambapo Waziri Mkuu huyo wa Italia analidharau tatizo la deni la nchi yake, wenzake kwenye serikali wanajitayarisha kuchukua hatua kubwa za kuiokoa nchi yao isisambaratike kiuchumi.

Hivi leo (14 Septemba 2011) Bunge la nchi hiyo linatarajiwa kuupigia kura mpango wa kwanza wa ukataji kodi na kubana matumizi. Ama ikiwa mpango huo wa euro bilioni 54 utapita au la, Berlusconi anaonekana kuyaunganisha masuala ya uhalisia wa deni na matarajio yake na imani yake binafsi.

Mwandishi: Tilmann Kleinjung/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo