1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, wasafirishaji haramu wa binadamu ni akina nani?

5 Julai 2023

Takriban asilimia 90 ya watu wanaovuka mipaka na kuingia ndani ya mataifa ya Umoja wa Ulaya kinyume cha sheria hutumia wasafirishaji haramu. Ni akina nani na hufanya vipi shughuli zao?

https://p.dw.com/p/4TSjq
Migranten wagen trotz Unfällen die Mittelmeerüberfahrt
Picha: Oliver Weiken/dpa/picture allianc

Wakala wa Umoja wa Ulaya wa kutekeleza sheria Europol umekadiria kuwa asilimia 90 ya wahamiaji wanaoingia Ulaya kinyume cha sheria hufanya hivyo kwa usaidizi wa wasafirishaji haramu- aidha katika safari yao nzima ama sehemu ya safari hiyo.

Bunge la Ulaya lilisema katika ripoti yake ya mwaka 2021 kuwa, "ni vigumu kupata takwimu halisi juu ya idadi hiyo, hasa kutokana na usiri katika mchakato mzima wa uhamiaji."Italia na Poland zataka ufumbuzi wa mzozo wa wahamiaji

Ni ukweli usiofichika kwamba, wasafirishaji haramu wanafanya biashara inayowapa faida kubwa. Ripoti hiyo ya bunge la Ulaya imeendelea kueleza kuwa licha ya uhamiaji kufanywa kama biashara, wapo wahamiaji ambao huingia ndani ya Umoja wa Ulaya kwa njia za halali na zinazokubalika kisheria.

Hata hivyo, swali kuu linaloibuka ni kwanini wahamiaji haramu wamekita oparesheni zao zaidi katika bahari ya Mediterania? Ni akina nani wanaotegemea huduma zao kuwafikisha Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha bora?

Usafirishaji haramu wa binadamu ni nini?

Lucia Bird, mchambuzi mkuu wa taasisi ya kimataifa dhidi ya uhalifu uliopangwa amesema usafirishaji kwa njia ya magendo unahitaji mtu kuvuka mipaka ya kimataifa, na kuhitaji watu kulipia safari hiyo.

Wahamiaji wa Tunisia
Wahamiaji wa kiafrika ambao wengi wanajaribu kuingia UlayaPicha: Hasan Mirad/Zumapress/picture alliance

Bi Bird, kutoka taasisi hiyo huru ya kiraia nchini Uswizi ameiambia DW, na hapa namnukuu, "Usafirishaji haramu wa binadamu ni kinyume cha matakwa ya mtu na hali hiyo inaweza kutokea hata ndani ya nchi.”

Ameongeza kuwa, aghalabu wahamiaji hukabiliwa na unyanyasaji mkubwa miongoni mwa wasafirishaji hao haramu licha ya safari hiyo kuanza kwa mkataba wa hiari kati ya mhamiaji na msafirishaji.

Huko Pakistan pia: Pakistan yawakamata watu 10 kwa kuuza binadamu

Mchambuzi mkuu huyo wa taasisi ya kimataifa dhidi ya uhalifu uliopangwa anaeleza kuwa, mara nyingi wahamiaji wanaotumia mtandao wa wasafirishaji haramu hufanikiwa kukwepa nyavu za walinzi na hatimaye kuvuka mipaka ya kimataifa.

Kulingana na ripoti ya uhamiaji ya watu duniani, takriban watu milioni 281 wanachukuliwa kuwa wahamiaji wa kimataifa mnamo mwaka 2021- idadi hiyo ni asilimia 3.6 ya idadi jumla ya watu duniani.

Je, wasafirishaji haramu hufanya kazi vipi?

Wasafirishaji haramu ni watu wenye mtandao mkubwa kwa ajili ya kutoa huduma za kuwasafirisha watu kutoka sehemu moja na kwenda nyengine. Ili kufanikisha hilo, wasafirishaji hao huwatumia watu kutuma ujumbe kutoka ngazi ya vijijini, ambao nao hushirikiana na wasafirishaji hao kuwafikisha wahamiaji karibu na maeneo ya mipakani. Kuna watu ambao pia kazi yao kubwa ni kugushi stakabadhi muhimu, pamoja na kukodisha boti na kuratibu mipango ambayo inatajwa kuwa muhimu katika kufanikisha safari yenyewe.

Ajali za kuzama kwa boti: Watu 500 wahofiwa kufariki katika ajali ya boti Ugiriki

Bi Bird ameeleza kuwa, wasafirishaji haramu hutoa suluhu kwa vikwazo vya asili au vile vya kisiasa ambavyo ni vigumu kuvikwepa pekee yako, kwa mfano kusaidia mtu kuvuka bahari ya Mediterania au kupata visa au vyeti vya usafiri kwa njia ya ulaghai.

Naye Said Hamdi, mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kijasusi lenye makao makuu yake mjini London anasema kuwa, moja ya sababu za mafanikio ya mtandao huo wa usafirishaji wa watu hasa nchini Tunisia na Libya, ni kutokana na wao kufanya kazi katika mazingira wezeshi.

USA | Texas |
Mwanamke mwamiaji akiwa amebebwa baada ya kushindwa kupumua baada ya kukosa hewa huko MarekaniPicha: Kaylee Greenlee Beal/REUTERS

Kipi kinachochangia uhamiaji?

Hamdi ameongeza kuwa machifu na maafisa wa serikali za mitaa hupewa hongo na kufumbia macho shughuli hizo za usafirishaji wa watu. Lakini pia maafisa hao wa serikali huonekana kuwa wepesi kuruhusu tabia hiyo kuendelea wakitoa sababu ya kuwapa fursa watu kutafuta maisha bora barani Ulaya.

Ingawa kifungu cha 14 cha azimio la kimataifa la haki za binadamu kinasema kwamba, "kila mtu ana haki ya kutafuta hifadhi au sehemu salama ya kuishi kutoka kwa mazingira yasio salama na mateso,” sio kila mhamiaji anafuzu kupata hifadhi chini ya mfumo wa sasa wa kisheria wa kuomba hifadhi. Mchakato wa kuomba hifadhi huanza pindi mtu anapofika kwenye mipaka ya Umoja wa Ulaya, kwa mfano baada ya kuvuka bahari ya Mediterania na sio kabla.

Safari hatari za bahari ya Mediterania kwenda Ulaya

Nadia Hardman, mtafiti wa haki za wahamiaji katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch anasema, "Watu ambao hawana nafasi ya kuchagua maisha mazuri na yenye hadhi ya juu, hujitoa kimasomaso na kuamua kusafiri kwa kutumia njia za hatari.”

Sikiliza: 

Bi. Hardman anahisi kuwa, safari hizo ambazo mara nyingi zinaonekana kufanywa kwa hiari japo kinyume chake ni kwamba sio za hiari bali watu hulazimishwa.

Anaongeza kuwa, hakuna mtu anayetaka kuondoka nyumbani kwao lakini kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, baadhi hugeukia fursa yoyote inayojitokeza mbele ili kuondokana na mzigo mzito wa maisha.

Hata hivyo, baadhi ya wahamiaji hudhulumiwa kimapenzi au kunyanyaswa kwa kukosa fedha kamili za kugharamia safari yenyewe, na wakati mwingine huchukuliwa kama watumwa kama sehemu ya kulipa deni. Baadhi ya wahamiaji hao, hulazimishwa kufanywa kazi za mikono katika miji ya mipakani ili kulipa deni.