1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Olmert asema hatawaachilia huru wafungwa wa kipalestina

5 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD65

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert amemwambia waziri wa nje wa Marekani Condoleezza Rice kwamba Israel haitawaachilia huru wafungwa wa Palestina kabla wanamgambo kumuachilia huru mwanajeshi wake anayezuiliwa huko Gaza.

Taarifa ya serikali mjini Jerusalem imesema kuwaachilia huru wafungwa wa kipalestina kutalipa nguvu kundi la Hamas liongeze masharti yake ya kumuachilia koplo Gilad Shalit.

Ehud Olmert jana amemwambia Condoleeza Rice wakati wa chakula cha jioni katika ikulu yake mjini Jerusalem, kwamba yuko tayari kumsaidia rais wa Palestina, Mahmoud Abbas. Aidha Olmert amesema Israel itakifungua kituo muhimu cha kibiashara cha Karni kilicho mpakani kati ya Israel na Ukanda wa Gaza.

Bi Condoleezza Rice aliwasili Jerusalem akitokea Ramallah ambako alikutana na rais Mahmoud Abbas.

Rice alisema Marekani ina wasiwasi mkubwa juu ya hali mbaya inayowakabili wapalestina. Akizungumza katika mkutano na waandashi habari pamoja na rais Abbas, Condoleezza Rice alisema Marekani itaongeza mara mbili juhudi zake kuboresha hali ya kimaisha ya wapalestina.