1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi wa DRC zatandwa na giza

23 Novemba 2011

Matukio wakati wa kampeni ya uchaguzi wa Novemba 28 Novemba kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanayafanya mashirika ya haki za binadamu yawe na wasiwasi wa vurugu kutokana na hotuba za chuki na ghasia.

https://p.dw.com/p/13FEh
Rais wa sasa na mgombea wa wadhifa huo, Joseph Kabila, wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.
Rais wa sasa na mgombea wa wadhifa huo, Joseph Kabila, wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.Picha: picture-alliance/dpa

Je uchaguzi huu utainufaisha demokrasia changa ya nchi hiyo au utairudisha kwenye giza la machafuko? Mmoja wa wanaogombea kiti cha urais kwa tiketi ya upinzani, tayari amekwishajitangaza kuwa yeye ndiye rais. Risasi zimekwishafyatuliwa na polisi kuwatawanya waandamanaji, na katika eneo la mashariki ambalo limekumbwa na mizozo mingi, waasi wamekuwa wakichoma moto madaftari ya wapiga kura, kuwazuia raia kwenda kwenye vituo vya uchaguzi.

Ni maoni ya wengi kuwa uchaguzi wa Novemba 28 utampa ushindi rais wa sasa Joseph Kabila, lakini vile vile wengi wanaamini kuwa hilo litatibua vurugu zaidi katika nchi hiyo kubwa zaidi kusini mwa jangwa la Sahara.

Nchi za Magharibi zimetoa mabilioni ya dola katika juhudi za kurejesha utengamano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Shirika linalofuatilia kwa karibu hali ya mizozo duniani, International Crisis Group, linasema kufaulu au kushindwa kwa uchaguzi ujao nchini humo, kutatoa muelekeo ima wa kuimarisha demokrasia yake changa, au kuitumbukiza tena nchi hiyo katika mzozo mwingine.

Shirika la Haki za Binadamu, Human Rights Watch, linasema vimetokea visa kadhaa vinavyowalenga watu kutoka jimbo la mgombea wa upinzani, Etienne Tchisekedi.

Mgombea wa upinzani, Etienne Tshisekedi (kushoto).
Mgombea wa upinzani, Etienne Tshisekedi (kushoto).Picha: Flickr/Foreign and Commonwealth Office

Mshirika wa Rais Joseph Kabila, Gabriel Kyungu, ambaye aliwahi kuwa gavana wa jimbo la Katanga, anashutumiwa kusema kuwa "kuna mbu wengi ndani ya sebule, na ni wakati wa kupulizia dawa ya kuua wadudu". Inasemekana alikuwa akizungumzia watu hao kutoka kwao Tshisekedi. Kyungu amekanusha shutuma hizo.

Katika kile kinachoonekana kama kutowajibika kwa mfumo wa sheria, kiongozi wa wanamgambo kutoka eneo la mashariki, Ntabo Ntaberi Sheka, yuko kwenye orodha ya wanaogombea kiti bungeni. Mtu huyo anashutumiwa kuamrisha ubakaji wa mamia ya wanawake, na shirika la Human Rights Watch linasema anapaswa kufikishwa kizimbani kwa vyovyote vile.

Kushindwa kumkamata mtu ambaye anajitokeza hadharani kuomba kura, ni ishara kuwa hata madhambi mengine ya kupindukia hayataadhibiwa.

Joseph Kabila alichukua hatamu za uongozi baada ya baba yake kuuawa. Alishinda uchaguzi wa mwaka 2006, na tangu hapo amelisukuma bunge kufanya mabadiliko katika sheria ya uchaguzi. Kulingana na mabadiliko hayo, uchaguzi wa rais utakuwa wa duru moja tu badala ya mbili.

Njia pekee ya wagombe wa upinzani kuweza kufua dafu ilikuwa kujiunga pamoja, lakini kutokana na tamaa za kisiasa kila mmoja wa wagombea kumi wa upinzani ameamua kwenda peke yake.

Katika uchaguzi uliopita, Joseph Kabila alipata kura nyingi kutoka majimbo ya mashariki, lakini sasa amepoteza uungaji mkono huko baada ya kukaribisha jeshi la Rwanda kuingia huko kutafuta waasi wa kihutu wa FDLR.

Kwenye sekta ya maendeleo Kabila amefanya makubaliano na China yenye thamani za mabilioni ya Dola, ambamo China itajenga miundombinu na kupata madini kutoka Kongo. Hata hivyo, ameshindwa kutekeleza ahadi zake za kuleta uwazi na kumaliza rushwa na ubadhilifu ambavyo vimeota mizizi.

Ripoti ya umoja wa mataifa juu ya vurugu wakati wa kampeni imelinyooshea kidole jeshi la polisi ambalo inasema linatumiwa na wanasiasa. Kitengo cha ujasusi na vyombo vya mahakama pia vimetupiwa lawama na ripoti hiyo.

Waziri wa Habari, Lambert Mende, alisema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliegemea upande wa upinzani.

Ripoti hiyo ilionya kuwa iwapo ukandamizaji na kukiuka sheria vitaendelea, kuna hatari ya watu na vyama kuishia kuchukua sheria mkononi, hali ambayo itahatarisha demokrasia na kuielekeza nchi kwenye machafuko baada ya uchaguzi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE
Mwandishi: Josephat Charo