1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yamkabidhi mtuhumiwa gaidi kwa jeshi la Marekani

Maja Dreyer27 Machi 2007

Kenya imemkabidhi mtuhumiwa gaidi wa kundi la Al Kaida kwa jeshi la Marekani ambalo lilimpeleka kwenye jela la Guantanamo. Hayo ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon. Mfungwa huyu, Bw. Abdul Malik, anatuhumiwa kufanya mashambulio mawili mjini Mombasa mwaka 2002 ambapo watu 13 waliuawa.

https://p.dw.com/p/CHHU
Hoteli iliyoshambuliwa mjini Mombasa mwaka 2002
Hoteli iliyoshambuliwa mjini Mombasa mwaka 2002Picha: AP

Kwa mujibu wa taarifa za Pentagon, mtuhumiwa Abdul Malik alikamatwa katika operesheni ya jeshi la Marekani dhidi ya Al Qaida nchini Afghanistan, lakini uraia wake haukutajwa. Msemaji wa Pentagon, Bryan Whitman, alisema Bw. Malik aliungama kuhusishwa katika shambulio dhidi ya hoteli mjini Mombasa ambapo watu 13 waliuawa vilevile katika shambulio dhidi ya ndege ya shirika la Israel iliyokuwa ikisafirisha abiria 271 karibu na Mombasa. Mashambulio haya yote yalifanyika mnamo mwaka 2002. Afisa mwingine wa Marekani ambaye hakutaja jina lake aliongeza kusema kuwa Kenya ilitoa pendekezo Malik apelekwe Marekani. Kutokana na tuhuma za ugaidi alipelekwa Guantanamo.

Abdul Malik ni mfungwa wa kwanza kupelekwa Guantanamo tangu mwezi wa Septemba mwaka uliopita ambapo watuhumiwa magaidi 14 walipelekwa huko kutoka magereza ya siri ya CIA katika nchi nyingine wakiitwa watuhumiwa wa hali ya juu. Msemaji Whitman wa Pentagon alisema Malik ni mtu hatari lakini hakusema ni mtuhumiwa wa hali ya juu au kama inavyotamkwa kwa Kiingereza “high-value” . Maafisa wa Marekani wanatumia maneneo haya ikiwa wanaamini mtuhumiwa fulani ana umuhimu mkubwa katika operesheni za Al Qaida na ikiwa anaaminika anaweza kutoa habari muhimu.

Afisa mwingine wa Marekani ambaye pia hakutaka jina lake litajwe alisema Abdul Malik ni msaidizi wa Al Qaida katika eneo la Afrika Mashariki naye anajua watu muhimu wa mtandao huo wa kigaidi.

Kenya ilimkamata watu wengi wanaotuhumiwa kuwa ni wanangambo wa Kiislamu na wasaidizi wa mtandao wa kigaidi katika Afrika Mashariki tangu vita vya Somalia vilipoanza na kumaliza mamlaka ya Kiislamu mjini Mogadishu na katika kusini mwa nchi hiyo. Maafisa wa Marekani lakini hawakusema ikiwa Malik alikuwa mmoja wa wale wanamgambo waliokamatwa nchini Somalia. Lakini anaaminika kuwa na mahusiano na mtuhumiwa mwingine wa Al Qaida ambaye jeshi la Marekani linaamini amejificha kati ya wanamgambo wa Kiislamu waliokimbilia Somalia. Mtuhumiwa huyu, Mkenya Saleh Ali Saleh Nabhan anatafutwa kuhusiana na shambulio dhidi ya hoteli mjini Mombasa.

Abdul Malik ni mmoja kati ya wafungwa 385 wa Guantanamo. Wizara ya ulinzi wa Marekani Pentagon ilisema kuwa kesi dhidi ya Malik itasikilizwa kuamua ikiwa atafungwa kama mwanamgambo adui. Pentagon iliarifu kuwa kamati ya Kimataifa ya shirika la Msalaba mwekundu itaruhusiwa kumtembelea Malik.