1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatumbukia zaidi katika mzozo wa kisiasa

Josepaht Charo3 Januari 2008

Machafuko makubwa baada ya matokeo ya uchaguzi ni pigo kubwa kwa demokrasia nchini Kenya

https://p.dw.com/p/Cjss
Wafuasi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakiongeza kuni moto kuchoma kizuizi cha barabarani katika mtaa wa mabanda wa Kibera mjini NairobiPicha: AP

Kupuuzwa kwa miito iliyotolewa na jumuiya ya kimataifa kutaka kupatikane suluhisho la amani kwa mzozo nchini Kenya, kumeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Inakadiriwa watu 300 waliuwawa baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza rais Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu dhidi ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, katika machafuko yaliyozuka nchini humo. Watu wasiopungua 100,000 wamelazimika kuyahama makazi yao.

Shinikizo la kimataifa linaongezeka dhidi ya serikali na upinzani huku pande hizo mbili zikilaumiana kwa machafuko yanayoendelea nchini Kenya. Kwa mujibu wa takwimu rasmi rais Mwai Kibaki alimshinda mpinzani wake Raila Odinga kwa kura 230,000 na hivyo kuchaguliwa tena kuitawala Kenya kwa awamu ya pili.

Upinzani na waangalizi wa uchaguzi huo wanasema kulitokea mizengwe katika zoezi la kuhesabu kura na hata mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini humo, bwana Samuel Kivuitu, amekiri alishinikizwa na serikali ya rais Mwai Kibaki.

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ameitisha maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo hatua ambayo imesababisha mapambano makali kati ya polisi na waandamanaji. Machafuko yaliyosababisha maaafa makubwa nchini Kenya baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa ni pigo kubwa kwa demokrasia kwa nchi hiyo na hata nchi za bara la Afrika kwa ujumla.

Marekani ambayo ilikuwa ya kwanza kumpongeza rais Mwai Kibaki, ikisema alichaguliwa tena katika uchaguzi uliokuwa huru na wa haki, sasa imebadili msimamo wake na kuyameza maneno hayo huku ikitoa mwito suluhisho la amani la mzozo huo lipatikane chini ya upatinisho wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Kenya inaonekana kuwa mfano mzuri wa nchi iliyoendelea kiuchumi na yenye kuendeleza mageuzi licha ya kukabiliwa na visa vya ufisadi. Na huku ikipakana na Somalia, Kenya ni mshirika muhimu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa hususan katika eneo tete linalokabiliwa na hali ya wasiwasi.

Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye aliibadili katiba ya nchi ili aendelee kubakia madarakani, amempongeza rais Kibaki kwa kumshinda Raila Odinga. Hatua ya rais Museveni ni ishara mbaya kwa demokrasia katika bara zima Afrika.

Hatua ya viongozi wa serikali nyingine barani Afrika kunyaa kimya kuhusu udanganyifu uliotokea katika kuhesabu kura nchini Kenya inakumbusha kwa huzuni kubwa vurugu zilizosababishwa na rais Mugabe nchini Zimbabwe.

Mwito wa jumuiya ya kimataifa kutaka matokeo ya uchaguzi yahakikishwe unatakiwa kutekelezwa haraka iwezekanavyo na Umoja wa Afrika. Matarajio yanabakia kwamba ziara ya kiongozi wa umoja huo, rais wa Ghana, John Kufuor, imeahirishwa kwa muda tu.

Jumuiya ya kimataifa sasa inalazimika kumueleza wazi rais Kibaki kwamba hawezi kuendelea kuitawala Kenya baada ya kushinda katika uchaguzi uliokabiliwa na mizengwe. Mwito uliotolewa na baadhi ya wanasiasa kuitaka China, iongoze juhudi za upatanisho imezusha utata.

Hali ya wasiwasi ni kubwa kiasi kwamba machafuko yanayoendelea nchini Kenya huenda yakaenea katika nchi jirani, huku nchi hiyo ikiwa imepakana na bahari na ikiwa mapito ya bidhaa muhimu kwa nchi jirani.

Ikiwa nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda, Kenya inategemewa na nchi jirani kwa bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kupikia, chumvi na unga. Hata mafuta ya petroli yanayosafirishwa nchini Uganda, Rwanda, Burundi na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hupitia Kenya. Maeneo haya yote yamekabiliwa na uhaba wa mafuta.

Rais Kibaki ameitumbukiza nchi katika hali ngumu ambayo si rahisi kuitoa. Wananchi wamepoteza imani na kiongozi huyo ambayo huenda asiipate tena. Tofauti za kikabila nchini Kenya sharti ziondolewe haraka iwezekanavyo ili nchi hiyo isitimbukie zaidi katika machafuko.

Shinikizo la kimataifa dhidi ya rais Kibaki linatakiwa liongezwe ili akubali kuruhusu matokeo ya uchaguzi yathibitishwe kwa uhuru na uwazi na kumlazimisha afanye uchaguzi mpya.

Matokeo ya uchaguzi wa bunge uliofanyika sambamba na uchaguzi wa rais, yalitoa matumaini makubwa kwa Kenya kwani kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia, Wakenya walipiga kura na kuwaondoa wanasiasa wakongwe waliotumia madaraka vibaya, wenye ukabila na waliohusika katika ufisadi.