1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha 64 cha Baraza kuu la Umoja wa mataifa

Oumilkher Hamidou24 Septemba 2009

Hotuba ya Ahmedinedjad yasusiwa na mataifa kadhaa ya Umoja wa mataifa

https://p.dw.com/p/JnwO
Rais wa Iran M.AhmedinedjadPicha: AP

Dazeni moja ya wajumbe wanaohudhuria mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa,walitoka nje pale rais wa Iran Mahmoud Ahmedinedjad alipopanda jukwaani .Kabla yake kiongozi wa Libya Mouammar Kadhafi alilitumia jukwaa hilo hilo kuzikosoa nchi za magharibi.

Miongoni mwa walioupa kisogo ukumbi wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa ni pamoja na ujumbe wa Marekani ,Ujerumani,Uengereza,Ufaransa, Danemark,Argentina,Costa Rica,Uruguay,New-Zealand na Australia.

Katika hotuba yake,rais wa Iran Mahmoud Ahmedinedjad alizungumzia hali namna ilivyo ulimwenguni na kuwashamabulia moja kwa moja wamarekani na mayahudi.

"Si jambo linalokubalika hata kidogo kukiachia kikundi kidogo kidhibiti,siasa,uchumi na utamaduni wa ulimwengu mpana,eti kwasababu ya mitandao yake ya kisasa-kianzishe aina mpya ya utumwa na kufuja hadhi na sifa ya mataifa mengine,ikiwa ni pamoja na mataifa ya Ulaya na Marekani,ili kuyafikia malengo yake ya kibaguzi."Amesema hivyo rais wa Iran Mahmoud Ahmedinedjad.

Akiigusia Marekani na uamuzi wake wa kuingia Iraq na Afghanistan,kiongozi huyo wa Iran amesema "si jambo linalokubalika kutuma wanajeshi, umbali wa maelfu ya kilkomita,ili kupigana vita,kumwaga damu,pamoja na kueneza vitisho na hofu."

Hotuba ya rais wa Iran Mahmoud Ahmedinedjad imetolewa katika wakati ambapo viongozi wa madola makuu,wameelezea msimamo wao dhidi ya mpango wa kinuklea wa Iran .

"Ikiwa serikali za Iran na Korea ya kaskazini zitaamua kupuuza kanuni za kimataifa,ikiwa nchi hizo zitatanguliza mbele utaratibu wa kutengeneza silaha za kinuklea badala ya utulivu wa kimkoa,ikiwa zitadharau hatari ya mbio za kujirundikia silaha za kinuklea katika eneo la mashariki la Asia na mashariki ya kati,basi nchi hizo zitalazimika kujieleza." Alisema hayo rais Barack Obama katika hotuba yake mbele ya viongozi 120 wanaohudhuria mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa.

Onyo dhidi ya Iran limetolewa pia na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.Rais wa Urusi Dmitri Medvedev ambae hadi sasa alikua kimya linapozuka suala la vikwazo,amesema tunanukuu:"ni nadra kuona vikwazo vikileta tija,lakini katika baadhi ya kesi,vikwazo haviepukiki"Mwisho wa kumnukuu rais nwa Urusi.

UN-Generaldebatte in New York - Muammar al-Gaddafi
Kiongozi wa Libya Moammar GaddafiPicha: picture-alliance/ dpa

Mbali na Ahmedinedjad,kiongozi wa Libya pia,Muammar Gadhaffi amelitumia ujukwaa la hadhara kuu ya Umoja wa mataifa kuzikosoa nchi za magharibi.

Muammar Kadhaffi,aliyehutubia hadhara kuu ya Umoja wa mataifa kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani miaka 40 iliyopita,ametumia saa moja na dakika 35 ,badala ya dakika 15 anazopewa kila mjumbe,kutoa maoni yake kuhusu hali namna ilivyo ulimwenguni. Amefika hadi ya kulitaja baraza la usalama kua si chombo cha kidemokrasia.

Muammadr Gadhaafi ameyatuhumu madola makuu "kuanzisha vita vingi tangu mwaka 1945 ili kama alivyosema: "kuendeleza masilahi yao."

Ameshauri makao makuu ya Umoja wa mataifa yahamishiwe nchi nyengine.Na amezitaka nchi za Ulaya zililipe bara la Afrika mabilioni ya dala kutokana na madhara ya ukoloni.

Hotuba yake hiyo ambayo alizungumzia pia kuhusu kuuliwa rais wa Marekani,John F. Kennedy , vita vya Vietnam,mashariki ya kati,maharamia wa kisomali au chanjo, inaangaliwa kama haikua na kichwa wala miguu,alikua akichanganya kila kitu na kuyarudia mengine mfano katika suala la ukosefu wa haki ulimwenguni.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman