1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Lal Masjid atoa wito wa kujisalimisha

Mwadzaya Thelma5 Julai 2007

Majeshi ya usalama nchini Pakistan wametegua vifaa vya milipuko nje ya msikiti wa Lal Masjid uliotekwa ili kuwaonya walio ndani kujisalimisha.Milipuko hiyo imesikika mapema hii leo ikiwa ni siku mbili baada ya mapigano makali kutokea kati ya wanafunzi walio na msimamo mkali na majeshi ya usalama.Watu 16 wamepoteza maisha yao.

https://p.dw.com/p/CB33
Majeshi ya Pakistan nje ya msikiti wa Lal Masjid
Majeshi ya Pakistan nje ya msikiti wa Lal MasjidPicha: AP

Msikiti huo wa Lal Masjid umekuwa katika mstari wa mbele kwenye kampeni ya kulazimisha kufatwa kwa sheria za kiislamu za Sharia nchini Pakistan

Hapo jana mamia ya wanafunzi waliruhusiwa kuondoka kwenye msikiti huo baada ya kukaguliwa na polisi.Mmoja wa kiongozi wa ngazi za juu wa msikiti huo alikamatwa alipojaribu kutoka akiwa na mavazi ya kujigeuza ya kike.

Abdul Aziz aliyefanyiwa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni alivaa shela iliyogubika uso wake.Kwa mujibu wa kiongozi huyo takriban wanafunzi 250 wa kiume baadhi yao wakijihami kwa silaha vilevile 800 wa kike bado wako ndani ya msikiti huo wa Lal Masjid.

Bwana Abdul Aziz alikamatwa jana jioni pale alipojaribu kutoroka akiwa kwenye kundi la wanawake waliovaa burqa.Kwa mujibu wa maafisa wa serikali alitambuliwa kwasababu ya tumbo lake kubwa na urefu wake usio wa kawaida.

Yapata wanafunzi 50 wengine waliondoka kwenye msikiti huo hii leo ikiwa ni siku moja baada ya wengine 1200 kutoroka.

Serikali ilitangaza kuwa itasitisha agizo la kufyatua risasi kwa muda wa saa mbili.Agizo hilo la kuyatua risasi kila anapotokea mtu kwenye msikiti huo lilitolewa hapo jana.Majeshi ya usalama yaliendelea kuwashinikiza waliojificha msikitini kuondoka kabla alfajiri kwa kutegua vifaa 7 vya kulipuka.

Wanafunzi hao walilipiza kisasi kwa kurusha maguruneti kadhaa na risasi.Hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.Kituo cha televisheni cha kitaifa kilitangaza kuwa wanafunzi hao wajisalimishe au kuchukua jukumu la maafa yoyote yatakayotokea.

Kwa mujibu wa daktari mmoja katika Taasisi ya Utabibu ya Pakistan aliyezungumza na shirika la habari la AFP mwili wa mwanafunzi mmoja uliooza ulitolewa kutoka msikitini na mingine inaaminika kuwa bado imo ndani.

Kakake Aziz kwa jina Abdul Rashid Ghazi aliye naibu kiongozi wa msikiti huo mapema alikataa kujisalimisha kwa madai kwamba wafuasi alfu 2 bado wako pamoja naye.Aliongeza kuwa wao si magaidi kwahiyo hawahitajiki kujisalimisha ila kutafuta suluhu ya kuheshimika.Tareeq Azeem Khan ni waziri wa Habari na mawasiliano

''Kwahiyo tunasema kuwa watu hawa watapata msamaha kamili iwapo watatoka nje ya msikiti huo na kujisalimisha na tuna imani kuwa hatutahitajika kutumia nguvu ili walio msikitini watoke na kuwasilisha silaha walizo nazo kwa mashirika yanayohusika na kudumisha sheria vilevile watakaohusika na kusababisha vifo vya raia waso na hatia.''

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan anakabiliwa na tatizo la kisiasa huku uchaguzi mkuu ukisubiriwa kufanyika baadaye mwaka huu.Kiongozi huyo aliagiza wafuasi wa msikiti huo kusakwa baada ya kujaribu kulazimisha sheria za Taleban kufuatwa.Jaji mkuu alifurushwa kabla ya matukio yote hayo.Watu hao walioteka msikiti wa Masjid Lal wanaaminika kuwajumuisha wanamgambo wa Taleban kutoka maeneo yanayopakana na nchi ya Afghanistan aidha wa makundi ya kidini yaliyopigwa marufuku nchini Pakistan.

Kampeni ya watu hao katika msikiti huo wa Islamabad ilipelekea maafisa wa polisi kutekwa,watu wanaoaminika kuendesha madanguro vilevile kuvamia maduka ya kanda za muziki na video. Mvutano kati ya msikiti huo na serikali ulianza

Mwanzoni mwa mwaka baada ya wanafunzi wa kike kuchukua usimamizi wa maktaba ya watoto inayoendeshwa na serikali.Mwezi Aprili viongozi wa kidini walianzisha mahakama ya kiislamu iliyotangaza fatwa dhidi ya waziri mmoja wa kike.