1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa zamani wa Khmer Wekundu akamatwa

Maja Dreyer19 Novemba 2007

Viongozi wa serikali ya zamani ya Cambodia ya Khmer Wekundu, Khieu Samphan, amekamatwa leo mjini Phnom Penh na mahakama inayochunguza mauaji ya kimbari yaliyofanyika chini ya serikali hiyo katika miaka ya 70.

https://p.dw.com/p/CJLw
Khieu Samphan, akiwa na umri wa miaka 67
Khieu Samphan, akiwa na umri wa miaka 67Picha: AP

Mzee Khieu Samphan ambaye alikuwa kiongozi wa Cambodia wakati wa utawala wa Khmer wekundu ambaye sasa ana umri wa 76 leo, alikamatwa akiwa hospitalini katika mji mkuu wa nchi hiyo, Phnom Penh, na kupelekwa mahakamani. Ni mtu wa tano wa uongozi wa Khmer wekundu ulikuwa na msimamo mkali wa kikomunisti kukamatwa mwaka huu. Waliokamatawa kabla ni waziri wa mambo ya kigeni wa Khemer Wekundu na mke wake aliyekuwa waziri wa jamii pamoja na Noangh Chea ambaye alikuwa kiongozi wa itikadi na mkuu wa idara za ujasusi na gereza kuu Kang Kek Ieu anayejulikana kama Duch. Kulingana na mahakama inayochunguza uhalifu wa serikali hiyo ya Khmer wekundu, wote hao wanahusika na mauaji, maangamizaji, kufunga watu gerezani na utumwa na kuwalazimisha watu kufanya kazi. Dikteta wa zamani Pol Pot alifariki mwaka 1998.


Watu Millioni mbili inasemekana waliuawa chini ya uongozi wa kundi hili la Khmer wekundu kati ya mwaka 1975 na 79. Khmer ni jina la kabila la taifa la Cambodia. Wengine walipigwa risasi au kuuawa kwa njia nyingine, wengine walilazimishwa kufanya kazi ngumu iliyosababisha kufariki dunia. Watu wengi pia walikufa njaa. Watoto walitenganishwa na wazazi wao na kuwekwa kwenye kambi maalum ya elimu ili kulea jamii mpya. Pol Pot na kundi lake la “Khmer wekundu” walitaka kuunda jamii pya. Walipiga marufuku mali ya kibinafsi na fedha. Wakaazi wa miji walilazimishwa kuondoka nyumba zao na kuhamia mashambani na iliwabidi wananchi wote kuvaa nguo za aina moja tu za rangi ya nyeusi. Kila familia ilipoteza angalau jamaa mmoja au wawili katika muda huu mfupi. Katika gereza lao maarufu la Tuol Sleng watu waliteswa vibaya. Kati ya watu 10.000 saba tu waliookoka.


Tangu hapo, viongozi wa serikali hiyo waliishi kwa amani nchini mwao. Mwaka uliopita kuliundwa mahakama ya kuchunguza mauaji hayo ya kimbari baada ya mazungumzo magumu kati ya Cambodia na Umoja wa Mataifa. Hadi sasa, mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, inakabiliwa na migororo ya ndani na mashtaka ya rushwa. Kesi zinatarajiwa kuanza kusikilizwa katikati ya mwaka ujao.


Khieu Samphan aliyeteuliwa na Pol Pot kuwa kiongozi wa serikali anakataa kwamba serikali yake ilikuwa na sera za mauaji. Siku chache tu kabla ya kukamatwa, alichapisha kitabu kipya juu ya historia ya Kambodia. Humo, Bw. Khieu anakiri kwamba vifo vilitokea lakini hayakuwa mauaji ya kimbari. Tayari kabla ya hapo, kiongozi huyu wa zamani alisema hakujua juu ya maovu yaliyofanywa lakini alifuatilia ndoto yake ya kuwa na nchi nzuri ya kilimo.


Khieu Samphon alikuwa kiongozi wa kundi dogo la wanafunzi wa Cambodia walisoma kwenya chuo kikuu cha Paris, Ufaransa katika miaka ya hamsini. Huko alishikilia itikadi ya kikomunisti na baada ya kurudi nyumbani kujiunga na kundi la waasi ambao baadaye walijiita Khmer Wekundu.