1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoAustralia

Kombe la Dunia la Wanawake limevutia wengi

4 Agosti 2023

Shirikisho la soka Duniani FIFA limesema mashindano ya Kombe la Dunia la Wanawake yanayoendelea nchini Australia na New Zealand, yameshuhudia idadi kubwa ya mashabiki.

https://p.dw.com/p/4UnBL
FIFA Frauen-Weltmeisterschaft 2023 – Italien gegen Südafrika
Picha: Joe Serci/Sport Press Photo via ZUMA Press/picture alliance

Baada ya wiki mbili za mechi takriban 48 , mashabiki waliowasili viwanjani wamefikia milioni 1.2 ikiwa ni wastani wa watu 25,000 kwa kila uwanja, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 29 ikilinganishwa na Kombe la Dunia nchini Ufaransa katika hatua hii ya mashindano.

Soma pia: Nigeria yaiangusha Ireland Kombe la Dunia la Wanawake

Kiongozi mkuu wa soka la wanawake katika shirikisho la FIFA, Sarai Bareman amesema ana imani kwamba kufikia fainali watakuwa na zaidi ya mashabiki milioni 1.9 ambao watakuwa wamewasili viwanjani, huku akisisitiza kuwa hadi sasa mashindano hayo yamekuwa ya kuvutia na wamezidi kabisa matarajio yao.

Unyanyasaji wa wachezaji

FIFA Frauen Fußball WM Sambia Costa Rica Barbra Banda
Picha: Juan Mendez/AP Photo/picture alliance

Huku yakijiri Shirikisho la soka duniani FIFA  pia linachunguza malalamiko ya utovu wa nidhamu yanayohusiana na timu ya wanawake ya Zambia kwenye kombe la dunia la wanawake, na kuapa kutoa adhabu kali ikiwa itathibitishwa.

Ingawa FIFA haikutoa maelezo ya kina, lakini ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa malalamiko hayo yanahusiana na tukio la kocha Bruce Mwape kudaiwa kumshika matiti mchezaji.

Soma pia: Gianni Infantino ashindwa kuweka wazi dola za kimarekani 30,000 kwa wachezaji wa Kombe la Dunia

Madai ya unyanyasaji wa kijinsia katika timu ya wanawake ya Zambia yalienea kwenye mitandao ya kijamii mnamo mwaka jana na kuzuka tena mwaka huu wakati wa kombe la dunia huku kocha Mwape akiandamwa na maswali mengi.

Zambia ilitolewa katika hatua ya makundi ya michuano hiyo nchini Australia na New Zealand baada ya kupokea kichapo kutoka kwa Uhispania na Japan kabla ya kushinda mechi yake na Costa Rica.