1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea ya Kusini: Mshambulizi ya Kaskazini ni alama ya ubabe

Admin.WagnerD24 Novemba 2010

Hali ya wasiwasi baina ya Korea ya Kaskazini na ya Kusini inaongezeka baada ya nchi hizo mbili kushambuliana kwa mizinga kwenye mpaka baina yao, tukio ambalo limeushitua ulimwengu mzima.

https://p.dw.com/p/QGkZ
Moshi ukitanda katika anga la kisiwa cha Yeonpyeong kilicho kwenye mpaka baina ya Korea ya Kaskazini na Kusini, baada ya kisiwa hicho kushambuliwa na mizinga ya Korea ya Kaskazini hapo jana (23 Novemba 2010) Picha ya AP/Yonhap.
Moshi ukitanda katika anga la kisiwa cha Yeonpyeong kilicho kwenye mpaka baina ya Korea ya Kaskazini na Kusini, baada ya kisiwa hicho kushambuliwa na mizinga ya Korea ya Kaskazini hapo jana (23 Novemba 2010) Picha ya AP/Yonhap.Picha: AP

Leo Korea ya Kaskazini imesema kwamba Korea ya Kusini inayaharibu mafungamano yaliyokwishaanza kuengeka baina yao kwa uchokozi wa kijeshi usiokuwa na maana. Shirika la Habari la nchi hiyo, KCNA, limesema kwamba Korea ya Kusini inauhujumu mpango wa kuimarisha mahusiano ya kijamii, inauua moyo wa ushirikiano wa vyama vya Msalaba Mwekundu vya nchi hizo na, kwa makusudi, inajenga mazingira ya vita baina yao.

Lakini Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Korea, Stephen Brosworth, anaichukulia Korea ya Kaskazini kama mtoto mtundu ambaye hupiga wenzake kisha akalia yeye kuonesha kwamba si mkosa. Anaitupia lawama za moja kwa moja Korea ya Kaskazini katika mzozo huu na ameapa kwamba nchi yake itaendelea kusimama pamoja na mshirika wake, Korea ya Kusini.

Mapema asubuhi ya leo, Shirika la Habari la AFP liliripoti kugunduliwa maiti mbili katika mabaki ya majengo yaliyobolewa na mizinga ya Korea ya Kaskazini iliyopigwa jana katika kisiwa cha Yeonpyeong, na hivyo kufanya idadi ya watu waliouawa kutokana mashambuliano haya ya mpakani kuwa wanne kwa upande wa Kusini.

Kisiwa cha Yeonpyeong Agosti 2010
Kisiwa cha Yeonpyeong Agosti 2010Picha: AP

Msemaji wa jeshi la wanamaji la Korea ya Kusini amesema kwamba watu hawa wawili walikuwa ni miongoni mwa wafanyakazi 12 wa ujenzi wa kambi ya wanamaji. Wote wawili wanakisiwa kuwa na umri wa miaka 60.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye mwenyewe ni Mkorea, ameyaita mashambuliano haya kama tukio baya kabisa kutokea tangu kumalizika vita vya Korea vilivopiganwa baina ya mwaka 1950 na 1953.

Korea ya Kusini yenyewe inaamini kwamba mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake na Korea ya Kaskazini yalikusudiwa kumjengea taswira ya kibabe mtu anayetarajiwa kuchukuwa madaraka ya nchi hiyo, Kim Jong-Un, ambaye ni mtoto wa kiongozi wa sasa, Kim Jong-Il.

Waziri Mkuu wa Korea ya Kusini, Kim Hwang-Sik, ameliambia bunge la nchi yake kwamba mashambulizi ya kisiwa kilichoko kwenye Bahari ya Manjano yalipangwa na yaliratibiwa kwa makusudi.

"Kaskazini ilikuwa inakusudia kujenga taswira ya nguvu za kijeshi za mrithi wa utawala, Kim Jong-Un, kuimarisha umoja wa ndani kwa kujenga hasira za wananchi wake dhidi ya ulimwengu wa nje." Amesema Kim Hwang.

Kauli kama hii ilitolewa pia na waziri wake wa Ulinzi, Kim Tae-Young, ambaye baada ya mazungumzo yake na waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, alisema kwamba Korea Kaskazini ilifanya mashambuizi haya kama alama kwamba hakutakuwa na mabadiliko ya siasa zake za nje, hata baada ya mabadiliko ya utawala ambayo yanatarajiwa kufanyika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP

Mhariri: Othman Miraji