1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa Papa kwaliacha kanisa katika mshangao

Admin.WagnerD12 Februari 2013

Baada ya uamuzi wa Papa Benedikt wa 16 kujiuzulu hapo jana, kanisa katoliki limejikuta katika hali ambayo halijawahi kuwemo kwa kipindi cha takribani miaka 700. Swali kubwa sasa ni nini kinachofuata.

https://p.dw.com/p/17cfl
Kujiuzulu kwa Papa Benedikti wa 16 kumewashangaza wengi katika kanisa
Kujiuzulu kwa Papa Benedikti wa 16 kumewashangaza wengi katika kanisaPicha: Reuters

Ni washauri wachache tu walio karibu na Papa, ambao walijua mpango wake wa kujiuzulu kabla ya kutangazwa hadharani. Hata vigogo katika uongozi wa Vatican walistushwa na uamuzi wa Papa Benedikt wa 16.

Kardinali Angelo Sodano amesema uamuzi huo ulikuwa kama radi katika anga lisilo na mawingu. Naye Kardinali Paul Poupard wa Ufaransa amesema kuwa neno la kwanza katika risala ya Papa liliashiria kitu kisichokuwa cha kawaida, na alipoangalia watu waliokuwa karibu naye, aliona nyuso zilizoduwaa kwa mshangao.

Maoni mchanganyiko

Kuna maoni mchanganyiko miongoni mwa waumini
Kuna maoni mchanganyiko miongoni mwa wauminiPicha: AFP/Getty Images

Maoni miongoni mwa waumini wa kanisa katoliki wapatao bilioni 1.1 kote dunia, yamegawanyika. Kuna wale ambao wamesema uamuzi wake ni wa kishujaa, na utaleta nguvu mpya katika kanisa hilo linalokabiliwa na migogoro, na pengine kumaliza mtindo wa kuwachagua wakongwe kuliongoza kanisa hilo. Lakini pia wako wale ambao wamebaki na maswali yasio na majibu, wakishindwa kuelewa namna mtu mwenye wadhifa ambao unatajwa kupatikana kwa mwongozo wa roho mtakatifu, anavyoweza kufanya uamuzi wa kujiuzulu.

Ni vigumu kutabiri mrithi

Swali kubwa lakini ni nini kanisa katoliki litakifanya kuanzia tangazo la Papa lilipotolewa, hadi tarehe ya kujiuzulu rasmi ambayo ni 28 Februari. Mwandishi wa siku nyingi wa shirika la habari la kikatoliki, KNA, Ludwig Ring-Eifel, anasema hakuna anayeweza kulijibu swali hilo kikamilifu.

Tetesi zimeanza kuhusu nani atachaguliwa kuwa Papa mpya.
Tetesi zimeanza kuhusu nani atachaguliwa kuwa Papa mpya.Picha: AFP/Getty Images

''Hatuelewi kila kitu kitakachofanyika, tunachojua ni kwamba tarehe 27 Papa atapata nafasi ya kuwaaga waumini mbele ya hadhara kubwa mjini Roma. Baada ya hapo mchakato wa kumtafuta mrithi wake utaanza, kupitia utaratibu ule ule unaotumika ikiwa Papa amekufa. Maana yake, nafasi ijulikanayo kama kiti cha Petro itakuwa wazi, na kanisa litakuwa na siku kati ya 15 na 20 kumchagua Papa mwingine.''

Ama kutoka kwa viongozi wa dunia, maoni yamekuwa kuheshimu uamuzi wa Papa Benedikti wa 16, na kushukuru mchango wake katika kutafuta maelewano ya kimadhehebu.

Muda mfupi, changamoto nyingi

Miaka 8 aliyoushikilia uadhifa wa Papa ni moja ya vipindi vifupi katika historia ya wadhifa huo. Hata hivyo, kipindi hicho kilitosha kumpatia Papa Benedikti wa 16 maadui wengi, wakiwemo mashoga na wanaharakati wa kupambana na ugonjwa wa UKIMWI. Katika kipindi hicho pia kashfa nyingi za visa vya mapadre kuwanajisi watoto zilifichuliwa.

Uvumi kuhusu nani anaweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya ulianza mara tu baada ya Papa anayeondoka kutangaza uamuzi wake. Lakini, hata wale wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Vatikani, wametoa tahadhari kwamba si rahisi kutabiri nani atachaguliwa.

Vatican imesema inatarajia kuwa Papa mpya atajulikana kabla ya siku kuu ya Pasaka, ambayo ni tarehe 31 mwezi Machi, ingawa kila kitu kitategemea mkutano wa faragha wa makardinali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman