1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuwaingiza watoto katika majeshi ya serekali nchini Burma kunalaumiwa na Shirika la Human Rights Watch

31 Oktoba 2007

Utawala wa kijeshi wa Burma, baada ya kuyakandamiza malalamiko na maandamano ya watawa wa dini ya Ki-Budha, ingali bado iko madarakani. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa bado unajaribu kuwabinya .majenerali wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/C77N
Watawa wa dini ya Ki-Budha wanaandamana nchini Burma
Watawa wa dini ya Ki-Budha wanaandamana nchini BurmaPicha: AP

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Burma, Ibrahim Gambari, kutokana na habari za mabalozi wa nchi za Magharibi, anatazamiwa tena kusafiri hadi Rangun hapo jumamosi ijayo. Atajaribu kuipatanisha serekali ya nchi hiyo na upinzani. Lakini kabla ya ziara hiyo, jumuiya ya kupigania haki za binadamu duniani, Human Rights Watch, imerejea tena kuulaumu utawala wa kijeshi wa Burma.

Majeshi ya serekali yana shida huko Burma, vipi kujijenga na kuwajibika; ndio maana kila wakati kunaonekana watoto wakitumika ndani ya jeshi hilo. Hayo yametajwa katika ripoti ya karibuni iliochapishwa na Shirika la kupigania haki za binadamu duniani, Human Rights Watch. Mwandishi wa ripoti hiyo, Jo Becker, anasema:

+Karibuni tulimhoji mtoto mwenye umri wa miaka 11 aliyeandikishwa jeshini. Alikuwa na urefu wa mita 1.30 tu na uzito wake ulikuwa kilo 31. Na licha ya hayo, jeshi lilimchukuwa. Katika jeshi watoto wanapatiwa mafunzo kama yale wanayopewa watu wazima, tena wakiwa tangu umri wa miaka 12 wanapelekwa katika medani za vita. Wanalazimishwa kupigana dhidi ya majeshi ya chini kwa chini ya makabila katika maeneo ya mashambani na wanalazimishwa kufanya vitendo venye kwenda kinyume na haki za binadamu, kuvichoma vijiji au kuwalazimisha raia wahame na waende kufanya kazi kwa nguvu.+

Bwana Jo Becker wa Shirika la Human Rights Watch anasema watoto hao hukamatwa katika vituo vya gari moshi, vile vya mabasi au katika maeneo ya hadharani na, kupitia watu wa katikati, huingizwa jeshini.

Watoto hao wanapokamatwa, hutakiwa waoneshe vitambulisho vyao, na pale wanaposema hawana basi hutupwa magerezani au kuingizwa jeshini. Kwa njia hiyo watoto wengi, kupitia vitsiho au kutumiliwa nguvu, huingizwa jeshini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la kupigania haki za binadamu ni kwamba kuwaandikisha watoto katika jeshi kumezidi katika miaka iliopita, japokuwa viongozi wa kijeshi wa Myanmar, kama vile Burma inavoitwa rasmi, miaka mitatu iliopita waliunda kamati ya kiserekali ilioshikilia kwamba umri kwa kijana kuingia jeshini uangaliwe kuwa unabakia miaka 18.

Shirika la Human Rights Watch linahofia kwamba kuandikishwa watoto katika majeshi huko Burma kunaweza kuongezeka siku za mbele kwa vile tangu kufyetuliwa risasi watawa wa dini ya Ki-Budha, jeshi limekuwa halipendezi mbele ya macho ya wananchi, kuliko lilivokuwa hapo kabla.

+Jeshi lina tatizo la kutokuwa na watu wa kutosha. Kwa upande mmoja jeshi linahitaji kuimarishwa, lakini, kwa upande mwengine, linapoteza wanajeshi zaidi wanaolikimbia. Ndio maana kunazidi mbinyo wa kutaka waandikishwe wanajeshi wepya. Baada ya kushindwa vuguvugu la kidimokrasia mwaka 1988, jeshi liliimarishwa zaidi na hapo kukaanza kuandikishwa watoto jeshini. Wakati huo, jeshi likazidi kutopendwa na wananchi, na hadhi ya jeshi imekwenda chini. Kunazungumziwa juu ya ukatili unaotendwa dhidi ya wanajeshi, matendo mabaya wanaofanyiwa na malipo mabaya. Na ndio maana watoto zaidi wanaandikishwa waingine jeshini.+

Sio tu katika majeshi ya serekali kuna watoto, pia majeshi ya waasi wa makabila yalio wachache yanawaingiza watoto katika vikosi vyao. Lakini ripoti ya Human Rights Watch inasema waasi hawawatumii watoto wengi kama vile yanavofanya majeshi ya serekali.