1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuwepo kwa Rais Mugabe wagubika Mkutano wa Lisbon

8 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CZ1N
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anahudhuria mkutano wa Umoja wa Ulaya na Bara Afrika mjini Lisbon.Picha: AP

Takriban viongozi 80 kutoka Ulaya na Bara Afrika wamekusanyika Lisbon,Ureno kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Bara Afrika,ukiwa ni wa kwanza baada ya kipindi cha miaka saba.Mkutano huo wa siku mbili unaanza leo Jumamosi na unatazamia kuimarisha biashara na kuboresha ushirikiano katika sekta za uhamiaji na ulinzi wa amani.

Lakini kuwepo kwa Rais wa Zimbabwe,Robert Mugabe anaetuhumiwa na Umoja wa Ulaya kukiuka haki za binadamu,kumezusha hali ya mvutano.Waziri Mkuu wa Uingereza,Gordon Brown ameususia mkutano wa Lisbon kupinga kuwepo kwa Mugabe.Vile vile wapinzani wa Mugabe waliandamana mjini Lisbon kupinga kushiriki kwa kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa tawi la Uingereza la chama cha upinzani cha Zimbabwe MDC,bwana Ephraim Tapa amesema,wamevunjika moyo na Ureno,vile vile wamevunjika moyo na Umoja wa Ulaya kwa sababu walidhani kuna vikwazo dhidi ya Mugabe.Lakini wanachokiona ni Umoja wa Ulaya ukivunja vikwazo vyake vyenyewe.

Lakini Umoja wa Ulaya ukizingatia ushawishi wa China unaozidi kujiimarisha barani Afrika, umeondosha vikwazo vya usafiri dhidi ya Mugabe.Leo katika mkutano wa Lisbon,Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel na Rais wa Afrika Kusini,Thabo Mbeki watazungumza juu ya haki za binadamu na uongozi mzuri.