1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen yaweka rekodi ya mwanzo bora wa msimu

13 Novemba 2023

Bayer Leverkusen chini ya kocha Xabi Alonso inaendeleza mwanzo bora zaidi wa msimu wa Bundesliga katika historia waliporejea kileleni mwa jedwali kwa ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Union Berlin.

https://p.dw.com/p/4YkZ6
Bayer Leverkusen - 1. FC Union Berlin
Mchezaji wa Bayer Leverkusen Jeremie Frimpong, akibanwa na wachezaji wa FC Union Berlin Jerome Roussillon na Sheraldo Becker.Picha: David Inderlied/dpa/picture alliance

Ushindi huo unamaanisha Leverkusen wamejikusanyia pointi 31 kati ya 33 zinazowezekana baada ya mechi 11, sawa na rekodi iliyowekwa na Pep Guardiola alipokuwa Bayern Munich msimu wa 2015-16.

Soma pia; Leverkusen haitikisiki kileleni mwa Bundesliga

Ushindi wa Bayern 4-2 dhidi ya Heidenheim uliwafanya Bavarians kukaa kileleni mwa jedwali Jumamosi usiku lakini vijana wa Alonso walidhibiti mchezo Jumapili, wakishinda kwa mabao ya Alex Grimaldo, Odilon Kossounou, Jonathan Tah na Nathan Tella.

Alonso aliipongeza timu yake kwa "subira" akisema "tumeridhishwa sana na tulichofanya kuanzia mapumziko ya awali ya kimataifa hadi sasa,  michezo mingi ya ugenini na kila mchezo tunashinda."

"Hisia ni nzuri kwa sasa."

"Hilo lilikuwa wazi -- tofauti ya wazi kiviwango," kocha wa Union Urs Fischer aliiambia DAZN, akisema upande wake ulikuwa kwenye "vita vya kushuka daraja."

Wenyeji walipata bao la kuongoza baada ya dakika 24, Grimaldo akisimama kwenye eneo la hatari kabla ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Union Frederik Ronnow.

Soma pia: Union Berlin wapokea kipigo cha 3-0 nyumbani

Grimaldo, 28 ameitwa kujiunga na timu ya taifa ya Uhispania kwa mara ya kwanza wiki hii, huku akiwa na magoli sita katika Bundesliga tangu alipojiunga na Leverkusen akitokea Benfica.

Leverkusen sasa wameshinda 16 na kutoka sare mmoja kati ya 17 katika mashindano yote msimu huu.  Union Berlin, ambao walimaliza katika nafasi ya nne na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, walimaliza wikendi wakiwa chini ya jedwali, wakiwa wamepoteza mechi tisa mfululizo.

Leipzig yaipiku Dortmund

Deutschland Bundesliga RB Leipzig vs 1. FC Köln
Wachezaji wa Leipzig wakisherekea ushindiPicha: opokupix/IMAGO

Kwingineko Jumapili, RB Leipzig ilishinda 3-1 nyumbani dhidi ya Freiburg na kuipiku Borussia Dortmund hadi nafasi ya nne.

Mchezaji aliyejiunga kwa mkopo kutoka Paris Saint-Germain Xavi Simons alitangulia kufunga baada ya dakika sita pekee kwa Leipzig, lakini Merlin Roehl wa Freiburg alifunga bao pekee na kusawazisha mabao kabla ya kwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza.

Mshambulizi wa Ubelgiji Lois Openda aliipatia Leipzig bao la kuongoza kisha Christoph Baumgartner akafunga dakika moja baadaye na kuwapatia wenyeji ushindi.

Katika mechi nyengine Eintracht Frankfurt walitoka nyuma kwa mabao mawili na kuandikisha sare ya 2-2 dhidi ya Werder Bremen.

Mshambuliaji wa Bremen, Marvin Ducksch alisherehekea kuitwa katika timu ya taifa ya Ujerumani kwa mara ya kwanza kwa mkwaju wa penalti naye Rafael Borre akafunga na kuifanya Bremen kuongoza kwa mabao 2-0, lakini Ellyes Skhiri na Hrvoje Smolcic walifunga mabao ya kipindi cha pili na kurudisha pointi moja.