1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafikiano katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya

P.Martin9 Machi 2007

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alieshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya, amefanikiwa kuungwa mkono na viongozi wa umoja huo mjini Brussels,kuhusika na pendekezo la kupunguza gesi ya kaboni dayoksaidi inayochafua mazingira.

https://p.dw.com/p/CHIT
Kansela Merkel akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels
Kansela Merkel akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini BrusselsPicha: AP

Baada ya kufanywa majadiliano marefu,viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuendeleza miradi ya nishati mbadala.Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barroso amesema,matokeo ya mkutano wa kilele mjini Brussels,ni mpango mkubwa kabisa wa kuhakikisha nishati na kulinda mazingira.Viongozi wa nchi na wa serikali za umoja huo wamekubali kupunguza utoaji wa gesi ya kaboni dayoksaidi kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020.Ikiwa Marekani na China vile vile zitaunga mkono mradi huo,basi Umoja wa Ulaya utapunguza utoaji wa gesi hiyo kwa asilimia 30.Kwani duniani,China na Marekani ni wachafuzi wakubwa kabisa wa mazingira.

Kwa upande mwingine,kuambatana na makubaliano ya Mkataba wa Kyoto hapo mwaka 1997,Umoja wa Ulaya ulikubali kupunguza utoaji wa gesi ya kaboni dayoksaidi kwa asilimia 8 ifikapo mwaka 2012. Lakini hadi hivi sasa,nchi za umoja huo ziko mbali kabisa na malengo yaliyowekwa wakati huo ya wastani wa asilimia 6.5 na sasa hadi asilimia 20.Hata hivyo Kansela Angela Merkel ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya akisifu makubaliano yaliyopatikana siku ya Ijumaa alisema,hayo ni mafanikio ya hali ya juu ambayo yatahakikisha uwezo wa ubunifu.Na dhima ya Umoja wa Ulaya kuonyesha mfano,itaufanya umoja huo kuaminiwa katika jumuiya kimataifa.Kwa sababu hiyo,kanuni za makubaliano yaliyopatikana lazima zifuatwe aliongezea Kansela Merkel.

Suala hilo lakini lilizusha mabishano makali,kwani katika Umoja wa Ulaya,matumizi ya nishati ya kila nchi ni tofauti.Kwa hivyo baadhi ya wanachama wameshikilia kuwa kila nchi ifikiriwe kulingana na matumizi yake ya nishati. Wakati huo huo,Ufaransa ambayo ni mzalishaji mkubwa kabisa wa nishati ya nyuklia,imesema kwa vile nishati hiyo haichafui sana mazingira,basi jambo hilo lizingatiwe katika ulinzi wa hali ya hewa na nishati hiyo iwe katika kundi la nishati mbadala.Lakini Kansela Merkel amesema,nishati ya nyuklia si nishati mbadala.Akaongezea kwamba nishati mbadala ni sehemu tu ya jawabu na haitotosha kufikia malengo yaliyowekwa kuhifadhi mazingira.Vipi maamuzi yaliyopitishwa mjini Brussels yataathiri wakazi wa Umoja wa Ulaya katika siku zijazo itadhihirika baada tu ya kuwepo utaratibu mrefu wa majadiliano.