1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabingwa wa bara la Ulaya wapigwa mweleka, Bafana Bafana hoi

Sekione Kitojo17 Juni 2010

Mshangao mkubwa umetokea katika fainali za kombe la dunia nchini Afrika kusini , baada ya Uswisi kuwaangusha mabingwa wa bara la Ulaya Hispania , timu inayoonekana kuwa ni "Timu ya karne".

https://p.dw.com/p/NsiV
Mashindano ya kombe la dunia nchini Afrika kusini, yaanza kuonyesha maajabu. Vigogo vya soka havijaonesha umahiri wao. Hapa ni pambano kati ya Uingereza na Marekani, ambapo Uingereza haikuonesha cheche zake.Picha: DW-Montage/AP

Mshangao mkubwa wa kwanza katika fainali hizi za soka za kombe la dunia , 2010 nchini Afrika kusini, umetokea. Mabingwa wa Ulaya Hispania wamepigwa mweleka na timu ya Uswisi wakati hakuna aliyetarajia mambo yatakuwa hivyo. Hispania ililala lakini hatimaye, kwa bao 1-0. Wakati wote wa mchezo Wahispania walikuwa wakimiliki mpira na kupeleka mashambulizi langoni mwa Uswisi.

Mabingwa hao wa bara la Ulaya , wamekuwa wakielezwa kuwa timu ya karne, wakati wa kuelekea katika mashindano haya ya kombe la dunia, lakini Uswisi ilipambana na wimbi baada ya wimbi la mashambulizi na wakafanikiwa kuweka mpira wavuni kwa bao lililopachikwa na Gelson Fernandes katika dakika ya 52 mjini Durban.

Ni ushindi wa kihistoria amesema kocha mwenye uzoefu mkubwa Ottmar Hitzfeld na kuongeza, kuwa hatujaweza kuwalshinda Hispania kwa muda mrefu.

Tulijaribu, kucheza kwa karibu karibu na imara, ili kuweza kulinda lango letu vizuri na kujaribu kungojea nafasi tutakazozipata. Unapocheza na Hispania huthubutu kucheza kwa uwazi. Mtu hawezi kushambulia sana, badala yake unaweza tu kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Timu imecheza kwa makini sana na nimefurahishwa na uchezaji wa timu yangu.

Amesema hayo kocha wa Uswisi, Ottmar Hitzfeld. Kocha wa Hispania Vicente Del Bosque amekiri: Huenda hatukuonyesha uwezo wetu kamili kama timu. Leo haikuwa siku yetu, amesema . Tuna michezo miwili iliyobaki mbele yetu na itabidi kutafuta njia ya kushinda zote.

Mchezo wa kwanza wa kundi hilo ulikuwa kati ya Honduras na Chile na Chile ikatoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Honduras.

Lakini matumaini ya Afrika kuweza kuingiza timu zake katika duru ya pili ya michuano hii, yaliingia doa pale wenyeji Afrika kusini walipogaragazwa kwa kuchapwa mabao 3-0 na Uruguay. Diego Forlan ndie aliyechafua sherehe kwa upande wa bara la Afrika pale alipokomea mabao 2 kabla ya Alvaro Suarez kukamilisha huzuni kubwa kwa bara la Afrika.

Afrika kusini na kocha wake Mbrazil Carlos Alberto Parreira sasa ni lazima dhidi ya Ufaransa wafanye kweli, ili kupata ushindi dhidi ya Ufaransa iwapo watataka kuota ndoto ya kuingia katika robo fainali. Kazi hiyo ni nzito, na anafahamu hilo nahodha wa Bafana Bafana Aaron Mokoena.

Tunahitaji kujiamini. Natumai tutashinda, dhidi ya Ufaransa na kupata kujiamini tena. Tuna mchezo mmoja uliobaki. Tunapaswa kwa kweli kuonyesha ile hali ya kujiamini kwetu.

Michezo mingine hii leo mchana ni kati ya Argentina na Korea ya kusini, ambapo mshambuliaji wa pembeni Park Ji-Sung wa Korea ya kusini na mshambuliaji wa Argentina Carlos Teves, watakuwa mahasimu wakubwa hii leo katika mpambano huo licha ya kufahamiana vizuri tangu walipokuwa pamoja katika timu ya Manchester United nchini Uingereza.Na pia Ufaransa inatupa karata yake nyingine hii leo dhidi ya Mexico katika mchezo mwingine wa kundi A.

Mwandishi: Sekione Kitojo/ AFPE/DPAE