1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Madagascar yaidhinisha ushindi wa Rajoelina

1 Desemba 2023

Umoja wa Ulaya na Marekani zimetoa wito wa kimataifa kupunguza mvutano wa kisiasa nchini Madagascar baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wa rais Rajoelina wa uchaguzi mkuu mwezi uliopita sasa ataongoza muhula wa tatu.

https://p.dw.com/p/4Zggh
Madagaskar imemchagua tena Rais Andry Rajoelina
Rais wa sasa wa Madagascar Andry Rajoelina ametangaza mshindi baada ya mahakama kuthibitisha matokeo ya uchaguzi.Picha: RIJASOLO/AFP

Rajoelina mwenye umri wa miaka 49, ambae yupo tayari kuanza muhula wake wa pili wa uongozi, amesema ushindihuo ni wa kishindo na kwamba hatoruhusu ukosoaji dhidi yake utakaopelekea machafuko kwa taifa hilo. 

Wagombea 11 wa upinzani wa urais bado wanashikilia msimamo wao wa kutokuyatambua matokeo hayo kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na dosari chungunzima.

Soma zaidi:  ANTANANARIVO: Uchaguzi wa rais nchini Madagaskar

Kiongozi huyo ameeleza kuwa dhamira yake kuu ni kuwajali watu hasa maskini na ameahidi kuharakisha hatua ya kuruhusu uanzishwaji wa viwanda vipya. Rajoelina amefahamisha juu ya kufanyika mabadiliko kidogo katika serikali japo amesisitiza kuwa, timu ya ushindi haifai kufanyiwa mabadiliko mengi.

Mgombea urais Siteny Randrianasoloniaiko akishiriki zoezi la kupiga kura katika kituo cha kupigia kura huko Ivandry, Antananarivo, Novemba 16, 2023, wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Madagaska. Kura za maoni zilifunguliwa Novemba 16, 2023 katika uchaguzi wa rais wa Madagascar, ambao unasusiwa na wagombea wengi wa upinzani kutokana na wasiwasi kuhusu uadilifu wa kura.
Mgombea urais wa upinzani Siteny Randrianasoloniaiko akipiga kuraPicha: MAMYRAEL/AFP/Getty Images

Baada ya mahakama kuhalalisha matokeo hayo, mabalozi kutoka Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi nyingine wafadhili walionesha wasiwasi wao kutokana na mivutano iliyoshamiri kwenye kampeni.

Katika taarifa yao wajumbe hao wamesema, Rajoelina ni lazima afanye juhudi za ziada kurejesha imani itakayotoa nafasi ya mazungumzo, huku wakisisitiza juu ya mapendekezo yao ya mara kwa mara kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi kabla ya uchaguzi ujao. 

Mivutano ya kisiasa imeonekana kushamiri katika kisiwa hicho kwa miezi kadhaa, ambapo makanali wawili wa jeshi walishtakiwa kwa makosa ya kuchochea uasi kuelekea uchaguzi huo wa Novemba 16.

Mkuu wa jeshiWilliam Michel Andriamasimanana ametilia mkazo juu ya jeshi kuheshimu matokeo hayo ya uchaguzi.

Siteny Randrianasoloniaiko, aliyekuwepo kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais, aliwasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo. Randrianasoloniaiko anadai kuwepo kwa uchakachuaji wa matokeo ya urais na ununuzi wa kura.

Soma zaidi: Machafuko Madagaskar

Ni mara chache mno kwa taifa hilo la kisiwa kufanya uchaguzi bila ya kuwepo kwa mzozo wowote.

Wamadagascar wamchagua tena Andry Rajoelina
Wafuasi wa Rajoelina wakisherehekea ushindi wake.Picha: RIJASOLO/AFP

Mgogoro wa hivi karibuni uliibuka mwezi Juni, baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Andry Rajoelina alikuwa na uraia wa Ufaransa, na hivyo kusababisha kuibuka kwa hoja ya wapinzani wake kutaka aenguliwe katika nafasi ya kuwania kiti cha urais. 

Rajoelina mwenyewe alikanusha madai hayo na kujitetea kuwa, alichukua uraia wa Ufaransa ili kuruhusu watoto wake kusoma nje ya nchi.

Rajoelina atoa tamko baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wake

Kabla ya uchaguzi, wagombea wa upinzani walifanya maandamano karibu kila siku katika mji mkuu, Antananarivo huku maandamano hayo yakitawanywa na vikosi vya usalama kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.

Rajoelina alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 wakati rais aliyemtangulia alipoondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi. Baada ya kutoshiriki uchaguzi wa mwaka 2013 kutokana na shinikizo la kimataifa, alishinda tena kwenye uchaguzi wa mwaka 2018 na tangu wakati huo amekuwa madarakani katika taifa hilo ambalo ni moja kati ya nchi maskini zaidi duniani licha ya kuwa na utajiri wa maliasili.

Takribani asilimia 80 ya idadi jumla ya watu milioni 28 nchini humo wanaishi chini ya dola 2 kwa siku.